Timu ya Azam FC ya Tanzania imeaga mashindano ya washindi barani Afrika baada ya kufungwa na AS FAR ya Morocco kwa magoli 2-1. Azam ambayo ilikuwa inahitaji droo ya magoli au ushindi wowote ili kusonga mbele katika michuano hiyo imeshindwa kupata matokeo hayo na kuifanya Tanzania ibakie mikono mitupu katika michuano ya kimataifa mwaka huu. Azam FC ambayo ilianza mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kupata goli mapema kabla ya wapinzani wao kupitia John Bocco ilishindwa kuwazuia wapinzani wao na dakika ya 21 AS FAR walifanikiwa kurudisha goli na baadaye kuongeza goli la pili. Katika dakika za mwisho Azam walipata penati ambayo ingeiwezesha Azam kusawazisha lakini mpigaji John Bocco aliikosa hivyo hadi mwisho wa mchezo Azam 1-2 AS FAR. Mbali ya kutolewa katika michuano hii Azam bado inaendelea kuwa ni mfano kwa timu za Tanzania ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki katika michuano ya kimataifa na imefanikiwa kufika raundi ya pili na imetolewa kwa ushindani tofauti na tulivyozoea kwa timu za Yanga na Simba ambazo huwa zinatolewa kwa idadi kubwa ya magoli na timu za kiarabu au za Afrika ya magharibi. Tunaamini Azam FC watajipanga upya msimu ujao kwenye michuano hii na wataweza kufanya vizuri zaidi.
No comments:
Post a Comment