Friday, June 7, 2013

Kauli ya TFF kuhusu Kagame Cup nchini Sudan

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema kuwa ushiriki wa klabu za Tanzania kwenye mashindano ya Kombe la Kagame yaliyopangwa kufanyika kwenye miji ya Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini nchini Sudan unategemea tamko la Serikali ambayo kwa sasa inafanya tathmini ya hali ya usalama. Tenga, ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF, alisema tayari TFF na Serikali zimeshafanya mazungumzo, na Serikali imepewa taarifa zote muhimu kuhusu mashindano kwa ujumla, malazi ya klabu za Tanzania, uhakika wa usalama, usafiri wa ndani na mambo mengine muhimu hivyo kwa sasa Serikali inatathmini taarifa hizo kabla ya kutoa tamko. “Masuala ya usalama yako nje ya uwezo wa CECAFA. Kwa hiyo, kama Serikali itabaini kuwa hali usalama ya huko si nzuri, hatutaziruhusu na kama ikiona hali ni nzuri, itaruhusu,” alisema Tenga. “Jukumu la CECAFA (Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu vya Nchi za Afrika Mashariki na Kati) ni kuandaa mashindano na kupata uhakika wa usalama kutoka nchi mwenyeji. “Kama tukipata uhakika huo wa usalama, mashindano yanafanyika. Lakini nchi moja moja zinayo haki ya kuhoji usalama kwa kuwa ni wajibu wa Serikali hizo kujali maisha ya wananchi wake.” Tenga alisema kuwa mashindano hayo yalikuwa yafanyike Ethiopia, lakini katika dakika za mwisho nchi hiyo iliomba isiandae mashindano hayo hadi mwakani na ndipo Sudan ilipojitokeza kuokoa mashindano hayo. Alisema wakati wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) uliofanyika Mauritius, CECAFA iliitisha mkutano mkuu wa dharura na kupewa taarifa ya maandalizi ya mashindano hayo kutoka uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Sudan na wanachama wakaridhia baada ya kuhakikishiwa usalama. “Hivyo nchi wanachama wa CECAFA zimeridhia kushiriki baada ya kuhakikishiwa usalama, lakini kwa kuwa Waziri wetu ameonyesha wasiwasi kuhusu usalama wa Darfur, hatuna la kufanya zaidi ya kumsikiliza. Ni kauli ya kiongozi anayeonekana kuwajibika na ni lazima tusubiri tamko la Serikali baada ya uchunguzi,” alisema Tenga. Michuano hiyo inatarajia kuanza tarehe 18 Juni hadi 2 Julai na timu zinazoshiriki michuano hiyo kutaka Tanzania ni Yanga, Simba na Falcons (Zanzibar) 

No comments:

Post a Comment