Wachezaji wawili kutoka Tanzania wamechaguliwa miongoni mwa 50 waliofanyiwa majaribio nchini Uganda kwa ajili ya kuingia katika kituo cha kuendeleza vipaji (centre of excellence) kilichoko Doha nchini Qatar kupitia mpango wa kukuza vipaji wa Aspire Football Dream. Abdulrasul Tahir Bitebo (15) ambaye ni mshambuliaji kutoka Kituo cha Uwanja wa Karume, na Martin Omela Tangazi (14) ambaye ni beki kutoka Kituo cha Ukonga ndiyo waliochaguliwa kutoka Tanzania kuingia katika kituo ambapo watakaa kwa mwezi mmoja kabla ya kusaini mkataba rasmi wa kuendelezwa. Mpango wa Aspire Football Dream unafadhiliwa na Mtoto wa Mfalme wa Qatar katika nchi 16 duniani, na kwa hapa nchini uko chini ya Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). TFF ina jumla ya vituo 14 vya kuendeleza vipaji kupitia mpango huo wa Aspire Football Dream. Vituo hivyo ni Karume, Kigamboni, Tandika, Kawe, Ukonga, Kitunda, Mbagala, Magomeni, Makongo, na Tabata vilivyo katika Mkoa wa Dar es Salaam. Vingine ni Bagamoyo kilichopo mkoani Pwani, Morogoro, Arusha na Moshi mkoani Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment