Sergio Aguero ndiye mfungaji hodari wa klabu ya Man city, kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Barcelona hakuweza kucheza kutokana na majeraha ya mguu. Aguero amerudi dimbani wiki mbili zilizopita akicheza mechi za ligi na FA cup. Muda aliyopata kwenye mechi hizi hakika ni mazoezi tosha kuweza kuwakabili Barcelona usiku wa leo. Ubutu wa mabeki wa Barcelona inaweza kuwa ni njia rahisi kwa Aguero kuiwezesha timu yake kupata magoli na hata kuweza kusonga mbele katika michuano hii. Mbali ya Aguero, Man city pia itawategemea Yaya Toure, Nasri na Silva wakiwa kama wachezaji tegemezi kwenye sehemu ya kiungo, ambapo ni lazima wacheze kwa juhudi na uwezo wote ili kupunguza umiliki wa mpira wa Barcelona. Mchezo uliyopita ulikwisha kwa Barcelona kushinda goli 2-0, hivyo ili Man city wasongembele wanatakiwa kushinda zaidi ya magoli 2.
Kwa upande wa Barcelona, ingawa ni timu inayoonekana kama inachechemea kwenye ligi, bado ni timu tishio barani Ulaya na itashuka dimbani usiku huu ikiwa na machungu ya kufungwa kwenye mechi ya ligi jumamosi iliyopita. Ni timu chache sana ambazo zimeweza kuifunga Barcelona kwenye uwanja wake wa nyumbani ikiwa ni jambo ambalo si jepesi kutokana na umahiri wa wachezaji wake akiwemo Messi, Neymar, Xavi, Cesc na Iniesta. Mazingira haya yanaifanya Man city kuwa kwenye wakati mgumu sana kufikia malengo yao ya kufika hatua ya robo fainali. Ili kujua kitakachotokea usiku wa leo endelea kutembelea Michezoupdates.
No comments:
Post a Comment