Gazeti la Marca linaeleza kuwa klabu ya Liverpool ipo kwenye hatua za mwisho kumsajili mshambuliaji wa Lille, Divock Origi. Origi ni raia wa Ubelgiji na alionesha kiwango kizuri kwenye michuano ya kombe la dunia. Liverpool tayari wametuma ofa ya paundi mil 10 kwa klabu ya Lille na mazungumzo bado yanaendelea.
Dailymail limeripoti kuwa klabu ya Man utd ina mategemeo makubwa ya kumsajili winga wa Real Madrid, Angel Di Maria dhidi ya PSG ambao wamekuwa wapinzani kwenye usajili wa mchezaji huyu. Man utd wanaamini Di Maria atapenda kujiunga nao ikiwa ni klabu kubwa yenye mafanikio kuzidi PSG. Tayari kocha wa PSG, Laurent Blanc amekiri kuwa usajili wa Di Maria bado haujakamilika, kauli inayoipa nguvu zaidi Man utd.
Dailymail linaripoti kuwa jitihada za klabu ya Arsenal kumsajili Mario Balotelli zimefikia ukingoni. Taarifa hizi zinasema, Balotelli hataweza kuhama baada ya klabu za Arsenal na Ac Milan kushindwa kufikiana makubaliano. Kauli ya Rais wa Milan, Adriano Galliani aliyoitoa hivi karibuni kwa kusema usajili wa Mario kwenda Arsenal umefia kwenye maji ilikuwa ni uthibitisho tosha kuwa Arsenal imeshamkosa Balotelli.
Klabu ya QPR ipo kwenye hatua za mwisho kumsajili mshambuliaji huru wa Chelsea, Samwel Eto'o. Makubaliano ya awali yameshafanyika kati ya QPR na Eto'o kilichobakia sasa ni masuala ya mshahara kwani Eto'o anahitaji kulipwa paundi mil 3 kwa mwaka.
Arsenal + Man utd + Chelsea. Klabu tatu za England zipo kwenye kinyang'anyiro cha kuwasajili wachezaji hawa watatu wa Real Madrid. Benzima anahitajika na Arsenal baada ya usajili wa Balotelli kushindikana, Khedira anahitajika na klabu mbili Chelsea na Arsenal wakati Man utd inamhitaji Di Maria. Khedira ameshakubali kuhama na klabu ya Madrid imeonekana ipo tayari kumuuza baada ya kumsajili Kroos, lakini usajili wake umeendelea kuwa mgumu kutokana na dau kubwa la paundi mil 20 ambalo Real Madrid inahitaji. Mbali ya ada kubwa, pia mshahara wake wa paundi laki 150,000 anaopokea kwa sasa umekuwa kikwazo kwa klabu ya Arsenal ambayo mishahara yake ipo chini. Lakini mazungumzo bado yanaendelea na lolote linaweza kutokea kabla ya Agosti 31 mwisho wa usajili. Di Maria habari zake zimeshaelezwa kwa kina kabla ya habari hii.
Dailysport limehabarisha kuwa golikipa mkongwe wa Real Madrid, Iker Casillas ameendelea kuishinikiza klabu yake kumuuza kwa Arsenal, kwani hawezi kuendelea kukaa benchi baada ya kupata ushindani mkali kutoka kwa Diego Lopez. Casillas alishawajulisha viongozi wake nia ya kutaka kuhama, lakini uongozi wa Madrid umegoma kumuuza kwa kile kinachoelezwa kuwa ni lulu ya klabu.
Gazeti la Mundo limesema kuwa klabu ya Barcelona itamsajili Vermaelen wa Arsenal kama itashindwa kumpata beki wa PSG, Marquinhos. Barcelona imeshatuma maombi mara kadhaa kumsajili Marquinhos kabla ya kombe la dunia kuanza lakini klabu ya PSG imekuwa ngumu kumruhusu. Jitihada za kutaka kumsajili beki huyu zimeanza tena lakini kama PSG wataendelea na msimamo wao basi klabu ya Barca itahamia kwa chaguo lao la pili ambaye ni Vermaelen.
Marca limeripoti kuwa klabu ya Liverpool imeshatuma maombi ya pauni mil 14 ili kumsajili winga wa Bayern Munich, Xherdan Shaquiri. Shaquiri ambaye alikuwa majeruhi kwa muda mrefu kwenye msimu uliopita, hakuweza kupata nafasi ya kutosha kuichezea klabu yake. Lakini uwezo wa mchezaji huyu ulionekana kwenye michuano ya kombe la dunia akiwaakilisha nchi yake Uswis. Uwezekano wa Liverpool kumsajili mchezaji huyu ni mkubwa baada ya Bayern Munich kuonesha nia ya kutaka kumuuza.
No comments:
Post a Comment