Thursday, October 10, 2013

Eto'o akubali ombi la Rais kurudi timu ya taifa

Rais wa Cameroon, Paul Biya amemshawishi mwanasoka Samuel Eto'o kutafakari upya mipango yake ya kujiuzulu kutoka soka ya kimataifa. Mshambuliaji huyo wa Chelsea alikutana na wawakilishi wa Rais mjini Yaounde kujadili mustakabali wa mchezaji huyo kuhusu soka ya kimataifa. Baada ya maongezi, Eto'o alikubali kurudi na kuichezea Cameroon kwa mara nyingine. Hivyo anatarajiwa kwenda Ufaransa kujiunga na wenzake kujiandaa kucheza dhidi ya Tunisia mechi ya kufuzu kombe la Dunia Brazil mwaka 2014. 

Etoo mwenye umri wa miaka 32, mapema mwaka huu aliwaambia wenzake kuwa hatacheza tena soka ya nyumbani punde tu baada ya Cameroon kushinda dhidi Libya na kuingia katika awamu ya pili ya kufuzu kwa kombe la dunia. Licha ya uamuzi wake wa kuacha soka la kimataifa, kocha wa timu ya Cameroon Volker Finke alimteua Eto'o kuchezea timu ya taifa ya Cameroon dhidi ya Tunisia ingawa mwenyewe hakuwa ametoa taarifa rasmi. Eto'o amekuwa na uhusiano mbaya na maafisa wa soka nchini Cameroon katika siku za nyuma ikiwemo hata kuongoza timu ya taifa kwenye mgomo uliosambaratisha mechi ya kirafiki dhidi ya Algeria. Eto’o aliadhibiwa kwa kupigwa marufuku kucheza mechi 15 ingawa baada ya kukata rufaa alipunguziwa adhabu hadi mechi 8. Hata baada ya adhabu yake kumalizika alikataa kuichezea Cameroon kwa miezi kadhaa. Pia sio mara ya kwanza kwa Rais Biya kuingilia kati na kumzuia mchezaji kujiuzulu kutoka katika majukumu ya kitaifa.

No comments:

Post a Comment