Ashanti 1-1 Spice stars
URA 3 - 1 Clove Stars
Mbeya city 1-2 Chuoni
Timu za Ashanti United na Spice Stars ya Unguja leo zimetoshana nguvu baada ya kutoka sare ya goli 1-1 katika mchezo wa kuwania kombe la Mapinduzi ULIKOPIGWA Uwanja Amaan.
Ashanti ndiyo walikuwa wa kwanza kuandika goli katika dakika ya 22 kupitia kwa Ike Brighton raia wa Nigeria ambaye alipachika goli maridadi kutoka pembezoni mwa lango kufuatia kuingia ndani ya eneo la hatari kwa kasi na kuachua mkwaju wa juu kwa mguu wa kulia uliomshinda mlinda lango wa Spice Mohamed Silima.
Wauza mitumba hao wa Ilala Dar es Salaam wangeweza kuongeza la pili dakika nne baadaye pale Brighton alipmramba chenga Silima lakini Laurent Mugia akawa mzembe kuunganisha mpira langoni.
Kipindi cha pili kilikuwa cha Spice ambao walicharuka na kulishambulia lango la Ashanti kwa nguvu na jitihada zao zilizaa matunda dakika ya 80 pale Abdallah Seif Bausi aliposawazisha kwa mpira wa kichwa ambao mlinda lango Juma Mpongo alishindwa kuudhibiti mikononi.
Na kama si uimara wa Mpongo langoni basi Spice wangeweza kuondoka na ushindi kwa wachezaji wake hasa Yunus Roma walipoteza nafasi tatu muhimu za kupachika magoli.
Huko Pemba URA wamewanyanyasa wenyeji Clove Stars kwa kuwachapa magoli 3-1 wakati Mbeya City wamekiona cha moto kwa kukubali kichapo cha magoli 2-1 kutoka kwa wenyeji Chuoni. Usiku huu ni mabingwa watetezi Azam dhidi ya Tusker ya Kenya kuanzia saa mbili usiku. Taarifa hii ni kwa niaba ya Azam TV
No comments:
Post a Comment