Tuesday, April 30, 2013

Brandts,tutaendeleza ushindi mechi zilizosalia

Kocha mkuu wa Yanga mholanzi Ernie Brandts amesema pamoja na kuwa tayari wameshatangazwa mabingwa wapya, bado kikosi chake kitashuka dimbani kuhakikisha kinaendeleza wimbi la ushindi wa kusaka pointi tatu katika michezo iliyosalia.Brandts alisema "Wengi wanaona kwa kuwa tumeshatwaa ubingwa basi tutapunguza kasi ya ushindi, hilo kwetu hakuna, tunaendelea na mazoezi kujiandaa kuhakikisha tunashinda michezo yote iliyosalia na kumaliza ligi kwa rekodi nzuri kuliko timu zote". Yanga inacheza na Coastal Union jumatano ya wiki hii, mchezo utakaovuta mashabiki wa Yanga kwa wingi ili kushangilia ubingwa, katika mchezo wa awali uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana jijini Tanga, Young Africans iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union mabao yaliyofungwa na washambuliaji Hamis Kiiza na Didier Kavumbagu. Mechi hiyo namba 172 itachezeshwa na mwamuzi Simon Mberwa kutoka Pwani akisaidiwa na Said Mnonga na Charles Chambea wote wa Mtwara wakati mwamuzi wa mezani atakiwa Hashim Abdallah wa Dar es Salaam. Kamishna wa mechi hiyo ni David Lugenge kutoka Iringa. 


Viingilio Yanga vs Coastal union 

Viingilio katika mechi hiyo itakayoanza saa 10.15 jioni ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh. 8,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000 na tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mchezo. Uongozi wa klabu ya Yanga umewaomba wanachama, wapenzi na mashabiki wa timu ya Yanga kujitokeza kwa wingi siku ya jumatano (mei mosi) katika dimba la uwanja wa Taifa ili kuishangilia timu yao na kuendeleza shangwe ya kutwaa Ubingwa wa VPL msimu huu.

No comments:

Post a Comment