Nchi ya Qatar bado ipo kwenye wakati mgumu
wa kutekeleza ahadi zake ilizoahidi wakati wanaomba tenda ya kuandaa kombe la
dunia mwaka 2022. Kikwazo kikubwa kwenye maandalizi yao ni kutafuta teknolojia
itakayoweza kupoza joto ndani ya viwanja. Nchi ya Qatar iliyopo kwenye jangwa
hufikisha nyuzi joto 40 kipindi cha mwezi wa tano hadi wa saba nyakati ambazo
kombe la dunia hufanyika. Kwa joto linalofikia nyuzi 40 ni vigumu kutumia
uwanja kwa wachezaji na watazamaji kutokana na uchache wa hewa ndani ya
kiwanja. Kutokana na hali hii kamati ya maandalizi ya kombe la dunia 2022
nchini Qatar inahangaika usiku na mchana kuhakikisha technolojia ya kupoza
uwanja inapatikana mapema kabla viwanja havijaanza kujengwa ili kuifanyia
majaribio.
Huu ni mfano wa Uwanja utakao jengwa nchini Qatar kwa kombe la dunia ambao utakuwa na viyoyozi ili kupoza joto baadhi ya wachezaji wameshaanza kuponda viwanja hivi wakisema hawana mazoea ya kucheza kwenye viyoyozi lakini nchi ya Qatar imetoa ahadi ya kuweka viyoyozi vya teknolojia ya juu ambavyo havitaweza kuwafanya wachezaji kuadhirika |
Msemaji wa kamati ya kombe la dunia nchini
Qatar bwana Nasser Al-Khater alisema wameshaongea na baadhi ya makampuni ya
nchini Ujerumani ambayo yaliomba tenda ya kutengeneza nyenzo ya kupoza uwanja kwa
kutumia mionzi ya jua. Lakini hadi sasa Qatar bado inaendelea kuchambua
makampuni hayo ili kujua uwezo wao kabla ya kuchagua kampuni itakayo tengeneza teknolojia hiyo. Watu wengi wakiwemo wajumbe mbalimbali wa
FIFA walipendekeza michuano hiyo ya kombe la dunia mwaka 2022 ifanyike mwezi
disemba kipindi ambacho nchi ya Qatar itakuwa na hali nzuri ya hewa lakini
kamati kuu ya FIFA haikuridhia pendekezo hilo kwani litaharibu ratiba nyingi
ikiwemo za ligi mbalimbali duniani.
Hiki ni kiwanja kitakachojengwa jijini Doha, Qatar kati ya viwanja vitakavyotumika kwenye kombe la dunia. Uwanja huu ukikamilika ndiyo umetabiriwa kuwa uwanja mzuri kuliko yote ya soka duniani ukiwa umezungukwa na maji sambamba na sehemu za starehe. Kiwanja hiki pia kitatumia teknolojia ya mionzi ya jua kupoza joto |
Uteuzi wa Qatar kuandaa michuano hii
ilileta utata hadi kupelekea baadhi ya viongozi wa FIFA kuchunguzwa
ikisemekana kwamba walikula rushwa ili kuipigia ya NDIYO kwa Qatar ikiwa wanajua hali ya hewa hairuhusu, lakini, FIFA katika sababu zake za kuichagua Qatar ilisema Qatar imechaguliwa kuandaa michuano hiyo ili kuleta hamasa ya mchezo wa soka kwenye nchi za
mashariki ya kati na Uarabuni. Vilevile FIFA walisema
mashariki ya kati ndiyo sehemu ya dunia iliyobakia ambayo bado haijaandaa kombe
la dunia baada ya Afrika kuandaa mwaka 2010. Kikwazo kingine ambacho nchi ya Qatar inakumbana
nacho kwenye maandalizi ya kombe la dunia mwaka 2022 ni utamaduni tofauti
walionao ambao hauruhusu pombe, mavazi ya nusu uchi, machangudoa na klabu za
disko vitu ambavyo kawaida vinaambatana na kombe la dunia. Akilielezea jambo
hili msemaji wa kamati ya maandalizi ya kombe la dunia mwaka 2022 bwana Al-Khater alisema
wataangalia jinsi ya kufanya ikiwa vitu hivi vitakuwa ni lazima kuvifanya
kwasababu Qatar ina desturi zake ambazo lazima zilindwe na itakuwa vyema watu
wakazijua desturi za nchi za kiarabu ila ametoa ahadi kuwa mbali ya vikwazo
vilivyopo kombe la dunia nchi Qatar litafanyika na watu watafurahia kuliko za
miaka mingine.
No comments:
Post a Comment