Thursday, May 2, 2013

FIFA yatoa maamuzi ya mgogoro uchaguzi wa TFF

Raisi wa TFF, Leodegar Tenga leo amewaambia waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa shirikisho hilo kuwa kamati ya FIFA imeshapitia na kutoa maamuzi kuhusu swala la mgogoro wa uchaguzi wa TFF, na yafuatayo ni  mapendezo ya FIFA katika barua waliyowatumia TFF wiki hii 

Katika barua hiyo FIFA imeiagiza 
1.Kuunda vyombo sahihi (Kamati ya Maadili itakayokuwa na vyombo viwili ambavyo ni cha kutoa maamuzi ya awali na cha rufaa) ambavyo mamlaka yake yatakuwa ni kushughulikia masuala ya ukiukwaji wa maadili;
2. Kufanya mabadiliko ya katiba kwa kuzingatia uundwaji wa vyombo hivyo;
3.Kuanza upya kwa mchakato wa uchaguzi wa Kamati ya Utendaji kwa kufungua milango kwa wagombea ambao walishachukua fomu na wagombea wapya:
4.Shughuli hiyo ikamilike ifikapo tarehe 30 Oktoba 2013.

Katika kutekeleza hayo, TFF inatakiwa iitishe Mkutano Mkuu wa Dharura kwa ajili ya kufanya mabadiliko ya Katiba kwa ajili ya kuunda kamati hizo za maadili na Kanuni za Uchaguzi kabla ya kuendelea na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Kamati Mpya ya Utendaji. Katika maoni yake FIFA imeeleza kuwa katika mchakato, Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliwaengua au kupitisha baadhi ya wagombea kwa kubaini kuwa walikiuka Ibara ya 9 (7) ya Kanuni za Uchaguzi na pia Ibaray a 29 (7) ya Katiba ya TFF ambavyo vinahusisha suala la kufungua kesi mahakamani, kufuja fedha za shirikisho na ukosefu wa uwajibikaji wa pamoja. Hata hivyo, FIFA ilisema kuwa watu hao walitakiwa waadhibiwe kwanza na kamati husika (kamati za maadili) kabla ya kuenguliwa na kamati za uchaguzi za TFF. “Kutokana na ukosefu wa kamati za maadili matokeo yake, mmoja wa wagombea amekuwa akienguliwa kwenye uchaguzi kila anapombea bila ya kujua adhabu yake ni ya muda gani,” inasema barua hiyo ya FIFA. Rais Tenga ameagiza kuitishwa kwa kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji ya TFF kupokea maagizo ya FIFA na kupanga ratiba ya utekelezaji wake kwa lengo la kuhakikisha kuwa mchakato huu unatekelezwa mapema iwezekanavyo.

No comments:

Post a Comment