Klabu ya Azam FC iliyopo nchini Morocco kupambana na AS FAR
katika mchezo wa washindi barani Afrika imetaja sababu sita zitakazoifanya timu
hiyo ishinde kwenye mchezo wake, sababu hizo ni kama zifuatazo
MAANDALIZI MAZURI
Timu za Tanzania kwa miaka mingi zimekuwa zikishiriki
mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na CAF,
kwa Azam FC hii ni mara yake ya kwanza kupata nafasi hii. Lakini unaweza
kuona utofauti mkubwa wa maandalizi kati ya Azam FC na timu nyingi za Tanzania
na utofauti huo ndiyo unaoifanya Azam FC hadi sasa kuweza kucheza mechi tano
bila kupoteza mchezo hata mmoja. Azam FC baada ya kujua kuwa itawakilisha nchi
kwenye mashindano ya kimataifa iliamua kufanya juhudi za makusudi za kujiandaa
kwa kiwango cha mashindano hayo yanayoandaliwa na CAF. Azam FC ilifanya ziara
na kucheza mechi nane za kimataifa za kirafiki nje ya ardhi ya Tanzania,
ilikwenda Kinshasa Congo DRC na kushiriki Congo Charity Cup ambako ilitwaa
kikombe kabla ya kusafiri tena hadi
Nairobi ambako ilipata nafasi ya kucheza mechi nyingine tatu. Lengo la ziara
hizi ilikuwa ni kuwapa ukomavu na uzoefu vijana wake ili wanapokuwa kwenye
mashindano ya CAF hasa wanapocheza mechi za ugenini wasiwe na hofu. Hakika
matunda ya ziara hizi tunayaona kwani Azam FC imeshinda ugenini mechi zake zote
mbili za awali hadi sasa. Maadalizi ya Azam FC kwenye mashindano haya pia
yalihusisha utafutwaji na usajili wa wachezaji wenye viwangovya kuweza kucheza
na kuisaidia timu, uboreshwaji wa kambi ya mazoezi ya Chamazi mapema kwa ajili
ya kambi yanyumbani, ununuzi wa vifaa bora vya mazoezi na kadhalika.
UWEZO WA WACHEZAJI
Timu ni wachezaji, bila ya wachezaji bora wenye nidhamu,
viwango bora na malengo ni sawa na bure. Azam FC ililitambua hilo mapema hivyo
haikukurupuka kusaka wachezaji kwa mkupuo, usajili wa wachezaji kwa ajili
yamashindano ya CAF ulifanyika kwa umakini kwa muda mrefu huku klabu ikijiwekea
malengo ya kuwa na kikosi bora
kitakochoweza kupambana na kuvifunga vigogo vya soka la Afrika. Leo
ukiwaangalia wachezaji 25 wa Azam FC waliosajiliwa kwenye mashindano ya CAF
utaungana nami kuwa niwachezaji sahihi kwa mashindano haya. Wachezaji wa Azam
FC wana nidhamu na vipaji vya hali ya juu. Wote wana viwango vya kuweza kuwemo
kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania wafuatao ni mfano tu wa wachezaji
wa Azam kwenye safu ya ulinzi na wasifu wao
MWADINI ALLY; Golikipa chaguo la kwanza la kikosi cha timu
ya Taifa ya Zanzibar na sehemu ya kudumu ya kikosicha timu ya Taifa ya Tanzania. Ana uzoefu mkubwa wa
michezo ya kimataifa akiiongoza Zanzibar kushika nafasi yatatu mara mbili
kwenye mashindano ya CECAFA. Ni golikipa hodari ambaye Azam FC tunajivunia kuwa
naye
AISHI MANULA, utasemaje juu ya kipaji cha kijana huyu toka
Morogoro? Wengi wanamfananisha na
golikipa wa zamani wa Tanzania na Simba Mohammed Mwameja. Aishi anajiamini, ana
umbo zuri na kipaji kikubwa sana. Ndiyo maana haishangazi kwa nini yeye ni
golikipa namba moja wa timu za vijana za taifa na chaguo namba tatu la Taifa
Stars ya kocha Kim Poulsen
HIMID MAO; Ana miaka 20 tuu lakini ni mkongwe ndani ya
kikosi cha Azam FC, Himid ni kiungo mwenye sifa za kukaba ambaye sasa anacheza
kama beki wa kulia wa Azam FC. Hakuna aliyeshangaa jina lake lilipoitwa na Kim
Poulsen kuwa sehemu ya wachezaji 30 bora nchini wanaonyemelea nafasi za walio
timu ya Taifa. Himid Mao aliibukia kwenye mashindano ya Copa Cocacola na
baadaye kuwa nahonda wa timu za taifa za Tanzania chini ya miaka 20. Kabla ya
mwalimu wa wakati huo wa Azam FC Itamar Amorim kumpa nafasi kwenye kikosi cha
kwanza akitokea Azam Academy. Himid anafanya vizuri sana kwenye kikosi cha Azam
FC hadi sasa.
WAZIRI SALUM; huenda ndiye mchezaji mwenye kipaji kikubwa
cha kumiliki mpira kuliko wachezaji wote nchini Tanzania kwa sasa. Waziri
Salum, naye yumo kwenye daftari la kocha Kim Poulsen na ni mwanachama wa kudumu
wa kikosi cha Zanzibar heroes. Mguu wake wa kushoto ni kama mkono wa paka kwani
anaweza kufanya lolote na mpita kwa kutumia mguu huu. Ana mbinu za kukaba, ana
krosi za hatari na chenga za maudhi. Ni hadhina kubwa kwa Azam FC na taifa la
Tanzania
JOCKINS ATUDO; beki
bora wa ligi kuu ya Kenya KPL msimu uliopita Jockins Atudo alitua Azam FC wakati wa dirisha dogo
la Disemba mwaka jana ili kuimarisha ukuta wa Azam FC kwa ajili ya mashindano
haya. Tangia atue Azam FC Atudo amethibitisha kuwa waliomchagua kuwa beki bora
hawakukosea. Kocha wa zamani wa Harambee Stars James Nandwa alisema wakati
tunataka maoni yake juu ya atudo kabla ya kumsajili kuwa ukiwa na beki kama
Atudo unapata vitu viwili, kwanza uongozi ndani ya uwanja pili beki mwenye
kipaji, nguvu, kimo na kujitolea hakika kila kocha angependa kuwa na Atudo
kwenye kikosi chake
LUCKSON KAKOLAKI; labda ndiye mchezaji mwenye busara zaidi
kwenye kikosi cha Azam FC kiasi kwamba wachezaji wenzake wanamuheshimu na
kumkubali kama kaka. Busara hizi za nje ya uwanja pia unaweza kuziona ndani ya
uwanja mbapo Luckson amekuwa mhimili mkuu kwa Azam FC hasa pale eneo la ulinzi
linapokabiliwa na majeruhi. Kiwango chake cha uchezaji kimekuwa cha uhakika
wakati wote na hili alilithibitisha kwenye mechi ya awali dhidi ya AS FAR
ambapo aliingia katika dakika ya sita baada ya Atudo kuumia na kucheza kwa
ustadi mkubwa sana Luckson ni mchezaji mmoja wapo ambaye tunaweza kusema ana
damu ya bluu (yaani ana damu yenye rangi ya Azam FC)
DAVID MWANTIKA; Tanzania tumejaaliwa kuwa na mabeki wazuri
lakini hatujawahi kuwana beki wa kiwango cha David Mwantika tangia kuondoka
kwenye ramani ya soka kwa Boniface Pawasa. Mwantika hapitiki kwa namna yoyote
ile… Mwantika ana nguvu za asili na mwili uliojengeka. Wenyewe wanyakyusa wanamuita Bedui… Mwantika ana
spidi ya upepo na amekuwa maarufu ndani ya wachezaji wa Tanzania lakini alikuwa
na umaarufu mdogo nje kutokana na timu yake ya Prisons kutopewa nafasi sana na
vyombo vya habari. Lakini ukikutana na washambuliaji wa ligi kuu watakuambia
kuwa beki wanayemuogopa zaidi nchini ni David. Juzi kim Poulsen amemjumuisha
kwenye kikosi chake na bila shaka wala wasiwasi Mwantika atavuka kwenye kikosi
cha Young taifa Stars na kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Taifa Stars muda
si mrefu
Mbali ya sababu hizi zilizoelezewa juu Azam FC imezitaja
sababu zingine nne kuwa ni Uongozi Mzuri, benchi bora la ufundi chini ya
Stewart Hall,Mipango mizuri na dhamira ya kupata mafanikio. Hivyo uongozi wa
Azam FC umewataka Watanzania kuwa na imani na timu hiyo ambayo itacheza na AS
FAR ya Morocco jumamosi hii katika mchezo wa marudiano baada ya mchezo wa
kwanza kutoka droo ya bila kufungana jijini Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment