Yanga |
Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara Vodacom na mabingwa watetezi wa kombe la Kagame timu ya Young Africans imeendelea na mazoezi katika uwanja wa shule ya sekondari Loyola kujiandaa na mashindano ya kombe la Kagame 2013/2014. Young Africans ambayo ilianza mazoezi tangu wiki iliyopita, inaendelea kuimarika kutokana na wachezaji wote kufanya mazoezi isipokua wachezaji waliopo katika timu za Taifa wakitumikia majukumu ya nchi zao. Kocha Brandts akiongea mara baada ya mazoezi alisema anashukuru vijana wake wako katika hali nzuri, kikosi kinaendela kujifua na wachezaji wote wako fit kiakili, kiafya na hakuna majeruhi hata mmoja hivyo ni nafasi nzuri kwangu kuweza kutoa mafunzo kwa wachezaji wangu. "Tumeanza mazoezi wiki iliyopita hapa hapa katika uwanja wa shule ya Sekondari Loyola, tunajianda na mashindano ya kombe la Kagame huku tukisibiria taarifa rasmi ya serikali juu ya usalama wa nchi ya Sudan, lakini pia tunatumia fursa hii kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom 2013/2014" alisema Brandts Aidha Brandts amesema kwa sasa anawakosa wachezaji wake zaidi ya nane waliopo katika timu za taifa kwa majukumu ya kuziwakilisha nchi zao lakini anaamini kufikia jumatatu ijayo wachezaji hao watakua wameshamaliza michezo yao na kujiunga na mazoezi ya klabu yao. Mashindano ya Kagame mwaka huu yamepangwa kufanyika nchini Sudan katika majimbo ya Darfur - Kaskazini katika mji wa Al - Fashir na Kordufuan Kusini kwenye mji wa Kadugli kuanzia tarehe 18 Juni 2013. Mapema Mei 10 mwaka huu klabu ya Yanga ililiandikia barua Shirikisho la Soka nchini Tanzania (TFF) kuulizia juu ya hali ya usalama, malazi na huduma zote watakazopatiwa timu ya Yanga ikienda nchini Sudan, lakini mpaka serikali inatamka bungeni juu ya hali ya Sudan walikua bado hawajajibu barua hiyo.
Kibaden-Kocha wa Simba |
Lakini wakati Yanga wakiwa kwenye mazoezi rasmi ya kujiandaa na michuano hiyo, klabu ya Simba bado inaendelea na msimamo wake wa kutoshiriki kwenye michuano hiyo kutokana na usalama kuwa mdogo nchini Sudan. Aden Rage mwenyekiti wa klabu ya Simba ndiye alianza kutoa taarifa za Simba kutoshiriki kwenye michuano hiyo, lakini vilevile kocha wa klabu hiyo Abdallah Kibaden pia alithibitisha uamuzi huo wa Simba na kusema anaupongeza uongozi wa Simba kwa maamuzi hayo na muda huu yupo kwenye harakati za kufanya usajili na hivi karibuni wataanza ziara za kwenda mikoani kucheza mechi za kirafiki ili kuwapima vijana wanaotarajiwa kusajiliwa na Simba kwa msimu ujao. Lakini taarifa ya TFF wiki iliyopita imesema klabu za Simba na Yanga ziendelee kujiandaa na michuano hiyo huku zikingojea taarifa ya serikali kuhusiana na usalama wa Sudan, na kama serikali ikisema kuna usalama klabu za Simba na Yanga zitatakiwa kwenda Sudan, na TFF ilisema taarifa hizo za serikali zitatolewa mapema kabla ya michuano hiyo haijaanza.
No comments:
Post a Comment