Kocha msaidizi wa klabu ya Simba Jamhuri Kihwelo "Julio" amesema kwasasa kamati ya ufundi wa klabu hiyo inafanya kazi kama Luku ya umeme. Kihwelo aliyasema hayo alipokuwa akiongea na EATV akiongelea mipango ya klabu hiyo iliyokuwa nayo kipindi hiki cha usajili. Kihwelo alisema ‘ Simba kwasasa tunajiita "Simba Luku" kwasababu tunafanyakazi kama Luku, mtu anavyolipia umeme ndivyo anavyotumia, hakuna ubabaishaji, hivyo na sisi kama benchi la ufundi tunaiga mfano wa Luku, kwamba yule mchezaji anayeonesha uwezo wake ndiye tutamsajili, na tukishamsajili anatakiwa kujituma uwanjani na kwenye mazoezi, akishindwa tunamuweka kando, vilevile, hatumchukui mtu aliyeletwa, hatujali hata kama ameletwa na kigogo, sisi tunaangalia uwezo wa mtu’. Mbali ya hayo, Kihwelo pia ametoa wito kwa wachezaji wote wanaopenda kujiunga na Simba wafike kwenye mazoezi yao ili kujitafutia bahati ya kuweza kusajiliwa na klabu ya Simba.
No comments:
Post a Comment