KLABU ya Simba imetoa taarifa kwa umma kuhusu Emmanuel Okwi. Katika siku za karibuni, vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini vimeripoti kuhusu uwepo nchini wa aliyekuwa mchezaji wa zamani wa klabu, Emmanuel Arnold Okwi kutoka nchini Uganda. Taarifa hizo zimeeleza mambo mbalimbali ikiwamo taarifa kuwa Simba Sports Club ina mawasiliano na mchezaji huyo na alikuja kwa mwaliko wa viongozi wa klabu. Baadhi ya vyombo vimekwenda mbali zaidi na kudai kuwa uongozi wa Simba unamshawishi mchezaji huyo avunje mkataba wake na klabu anayoichezea sasa ya Etoile du Sahel (ESS) ya Tunisia. Klabu inapenda kuuarifu umma kwamba Simba au kiongozi wake yeyote (Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Wajumbe wa Kamati ya Utendaji na Sekretarieti haijahusika kwa namna yoyote ile na ujio wa mchezaji huyo hapa nchini. Hakukuwepo na mwaliko rasmi au usio rasmi kwa viongozi wa Simba. Taarifa zozote za kuhusisha ujio wa Okwi na uongozi wa Simba ni za upotoshaji na zina lengo la kuharibu heshima na hadhi ambayo uongozi huu umeijenga kitaifa na kimataifa kwenye tasnia ya soka. Hata hivyo, kisheria, Simba haiwezi kumzuia mchezaji huyo kusafiri kwenda nchi yoyote anayotaka kama amefuata sheria zote za uhamiaji. Mchezaji huyo ana mkataba na timu nyingine na Simba haihusiki na safari zake, matembezi yake au mipango yake ya kimaisha. Uongozi wa Simba unafahamu kwamba Okwi ni mchezaji halali wa ESS maana wenyewe ndiyo uliomuuza kwa klabu hiyo. Kwa mujibu wa sheria za FIFA, klabu yeyote, ikiwamo Simba SC, haziruhusiwi kufanya mawasiliano na mchezaji huyo au yeyote yule halali wa klabu nyingine bila ruhusa ya klabu yake kama mkataba wa mchezaji husika umebakiza kipindi kinachozidi miezi sita. Hii maana yake ni kwamba uongozi hauwezi kumshawishi mchezaji huyo kujiunga na klabu.
No comments:
Post a Comment