Thursday, May 16, 2013

TPSC kidedea michuano ya Pro Life Mtwara

TPSC
Baada ya kukaa kwa muda mrefu bila ya ushindi dhidi ya Chuo cha Mtakatifu Agustino tawi la Mtwara (SAUT), Chuo cha Utumishi wa umma (TPSC) kimeweza kutoka na ushindi wa goli 2-1 dhidi ya SAUT katika mchezo wa mpira wa miguu uliofanyika kwenye uwanja wa Nangwanda mkoani Mtwara katika fainali ya Pro Life Competition 2013. Timu hizi mbili ndiyo zenye upinzani wa juu kwenye michuano hii na kawaida SAUT ndiyo watetezi wa kombe hili, lakini mwaka huu TPSC walijipanga vizuri na kuweza kuwadhibiti ipasavyo SAUT tokea mwanzo wa mchezo hadi mwisho. Michuano hii ambayo ni maarufu mkoani Mtwara inadhaminiwa na Father Aidan Msafiri ambaye ni mkufunzi katika chuo cha SAUT tawi la Mtwara. Chuo cha TPCS kiliingia fainali baada ya kukifunga chuo cha Uhasibu (TIA) tawi la Mtwara wakati SAUT waliingia fainali baada ya kuwatoa Naliendele Mtwara ambao ni kikosi cha jeshi kutoka jeshi la wananchi wa Tanzania tawi la Mtwara.  Wakati huo huo, kwa upande wa mpira wa pete SAUT tena ilipokea kichapo kutoka kwa TPSC lakini kwa upande wa volleyball SAUT iliweza kutetea kombe dhidi ya TPSC. Baada ya michezo hii kuisha baadhi ya wanafunzi wa chuo cha SAUT wamekiri kuondoka kwa wanachuo wenzao waliokuwa mwaka wa tatu kumezifanya timu zao kuwa dhoofu kwasababu hawakuwa wamejiandaa kupokea kijiti kutoka kwa wenzao waliomaliza. Michuano hii ya Pro Life inayodhaminiwa na Father Msafiri ilianzishwa ikiwa na dhumuni la kuwakutanisha pamoja wanavyuo na watumishi wa umma mkoani Mtwara ili kujenga umoja baina yao lakini vilevile kuendeleza michezo ndani ya mkoa na kuwafanya vijana wapate shughuli zingine za kufanya baada ya masomo na kazi ili kujiepusha na vishawishi vinavyopelekea maambukizi ya ukimwi.  

No comments:

Post a Comment