Tuesday, May 7, 2013

Yanga A na Yanga B zatoka droo ya goli 1-1

Timu ya Young Africans Senior (Yanga A) na timu ya  Yanga B almaarufu kama (U-20 ) leo zimetoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kirafiki (mechi mazoezi) wa kujipima kwa wachezaji wa timu hizo uliofanyika katika uwanja wa mabatini Kijitonyama leo asubuhi. Kocha Mkuu wa Young Africans mholanzi Ernie Brandts aliomba leo kuchezwa kwa mchezo huo ambao pamoja na kufanyika leo majira ya saa 2 asubuhi bado wapenzi, washabiki na wanachama walijitokeza kujionea uwezo wa wachezaji wao wa timu zao zote wakipimana ubavu. Young Africans Senior (A) iliyoongozwa na kocha Brandts ilijipatia bao la kwanza dakika ya 6 ya mchezo kupitia kwa mshambuliaji wake Hamis Kiiza 'Diego' ambaye aliukwamisha mpira wavuni akimalizia krosi safi ya Saimon Msuva. Kikosi cha kwanza cha Yanga A kiliendelea kulishambulia lango la timu B lakini walinzi wake wakiongozwa na nahodha Issa Ngao, Benson Michael walisimama imara kuhakikisha hawafungwi tena katika lango lao.

Timu B ililishambulia lango la A kupitia kwa washambuliaji wake Rehani Kibingu, Notikelly Masasi na George Banda lakini kutokua makini kwao kuliwakosesha mabao mawili ya wazi. Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zimalizika timu ya Yanga A ilikua mbele kwa bao 1-0. Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko ambao timu A ilibadilisha kikosi chake chote na timu B kubadilisha baadhi ya wachezaji wake. Mabadiliko hayo yalileta uhai kwa timu B kwani kiungo wa pembeni Abdallah Mbguli 'Messi'  aliipatia timu yake bao la kusawzisha baada ya kumalizia pasi nzuri ya kiungo Credo Wigenge  aliyewazidi ujanja walinzi wa timu A na kupiga pasi iliyomkuta Messi na kuukwamisha wavuni mpira huo. Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Timu A  1- 1 Timu B

Mara baada ya mchezo huo kocha mkuu Brandts alisema amefurahishwa na mchezo wa leo wa kirafiki kati ya timu ya wakubwa na wadogo, kwani amaepata fursa kuwaona wachezaji wake wote wa timu ya wakubwa na wadogo wakicheza kwa muda mrefu. Lengo la mazoezi haya leo ni kutoa fursa kwa wachezaji kucheza kwa muda mrefu,  kama unavyoona tumekuwa tukifanya mazoezi kwa takribani wiki nzima na bado tuna zaidi ya wiki mbili kabla ya mchezo wetu wa mwisho, hivyo ilikua ni vyema kuwaona wachezaji wangu wakicheza kwa muda mrefu kwani kutoka timu B nimeshafanikiwa kupandisha wachezai wanne timu ya wakubwa alisema 'Brandts' .Kikosi cha Young Africans kesho kitaendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo wake wa mwisho wa kukamilisha ratiba ya mzunguko wa pili dhidi ya watani wa jadi Simba SC mchezo utakaofanyika mei 18 katika dimba la uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Young Africans A : 1.Said Mohamed, 2.Mbuyu Twite/Godfrey Taita, 3.David Luhende/Oscar Joshua, 4.Nadir Haroub/Ladislaus Mbogo, 5.Kelvin Yondani/Shadrack Nsajigwa, 6.Athuman Idd/Omega Seme, 7.Saimon Msuva/Nizar Khalfani, 8.Frank Domayo/Nurdin Bakari, 9.Didier Kavumbagu/Jerson Tegete, 10.Hamis Kiiza/Said Bahanuzi, 11.Haruna Niyonzima/Stephano Mwasika.

Young Africans B:  1.Yusuph Abdul, 2.Zuberi Juma, 3.Said Mashaka, 4.Benson Michael, 5.Issa Ngao, 6.Omary, 7.Rehani Kibingu, 8.Credo Wagenge, 9.Noikely Masasi, 10.George Banda, 11.Abdallah Mnguli 

No comments:

Post a Comment