Upangaji ratiba (draw) ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) umefanyika leo (Mei 7 mwaka huu) huku mabingwa wa mikoa ya Dar es Salaam (Red Coast), Lindi (Kariakoo) na Kigoma (Saigoni) wakianzia nyumbani katika ligi hiyo itakayoanza Mei 11 au 12 mwaka huu. Ligi hiyo itachezwa kwa mtoano kwa mtindo wa nyumbani na ugenini ambapo mwenyeji atapanga tarehe ya mechi ambazo zinatakiwa kuchezwa kati ya Jumamosi au Jumapili. Mechi za marudiano katika raundi hiyo ya kwanza zitachezwa kati ya Mei 18 na 19 mwaka huu. Katika upangaji huo ulioshuhudiwa na waandishi wa habari kwa niaba ya klabu husika, mabingwa wa Mkoa wa Shinyanga (Stand Ngaya FC) wamepita moja kwa moja hadi raundi ya pili itakayochezwa kati ya Mei 25 na 25 mwaka huu wakati mechi za marudiano ni kati ya Juni 1 na 2 mwaka huu. Raundi ya tatu itachezwa kati ya Juni 8 na 9 mwaka huu wakati marudiano ni Juni 15 au 16 mwaka huu. Raundi ya nne itachezwa kati ya Juni 22 au 23 mwaka huu wakati marudiano ni Juni 29 au 30 mwaka huu. Raundi ya tano ni kati ya Julai 6 na 7 mwaka huu na marudiano ni Julai 13 au 14 mwaka huu.
Timu tatu ndizo zitakazopanda kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao, ambazo ni ya kwanza nay a pili wakati timu ya tatu itapatikana kwa timu zilizoshindwa hatua ya nusu fainali kucheza zenyewe kwa zenyewe. Washindi wa nusu fainali nao watacheza wenyewe kwa wenyewe ili kupata bingwa wa RCL ambaye atakabidhiwa kombe la ubingwa. Ligi hiyo inashirikisha mabingwa kutoka mikoa 27 ya kimpira ambapo katika raundi ya kwanza wanaanza mabingwa 26, raundi ya pili ni mabingwa 14 wakijumuisha na bingwa wa Shinyanga ambaye katika draw ameingia moja kwa moja katika hatua hiyo. Raundi ya tatu itashirikisha timu saba zilizosonga mbele pamoja na moja yenye uwiano mzuri wa matokeo ili kufanya jumla ya timu nane. Raundi ya nne itakuwa na timu nne. Wakati raundi ya tano itakuwa ni kumpata bingwa na mshindi wa tatu. Katika upangaji huo wa ratiba mechi za raundi ya kwanza (timu ya kwanza ikianzia nyumbani) itakuwa kama ifuatavyo; Red Coast vs Abajalo, Kariakoo vs Mtwara, Friends Rangers vs Kiluvya United, TECKFOLT FC vs African Sports, Machava FC vs Flamingo SC, Gunners United vs Manyara na Simiyu vs Magic Pressure FC. Nyingine ni Polisi Jamii Bunda FC vs UDC FC, Geita vs Biharamulo SC, Saigoni SC vs Tabora, Katavi Warriors vs Rukwa United, Mji Njombe vs Mbinga United na Kimondo FC vs Iringa.
Mechi zitachezwa katika viwanja vya makao makuu ya mikoa, vinginevyo kuwepo na maombi rasmi ambayo yatakubaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
No comments:
Post a Comment