Sunday, July 21, 2013

Rais wa Madrid amtembelea CR7 kumshawishi abaki

Rais wa klabu ya Real Madrid, Florentino Pérez akisalimiana na mshambuliaji wa klabu hiyo Cristiano Ronaldo leo asubuhi mahali klabu hiyo ilipopiga kambi nchini England. Ziara hii ya Perez ilikuwa maalumu kukutana na Ronaldo ambaye kwa muda walikuwa hawajakutana kutokana na wachezaji kuwa likizo. Perez pamoja na benchi la ufundi wapo kwenye mkakati wa kumshawishi Ronaldo asaini mkataba mpya na klabu hiyo ili kuondoa minong'ono iliyopo kuwa CR7 anaweza kuhama Madrid. 
Cristiano alionekana mwenye furaha kwa kutembelewa na Rais wa klabu, jambo linaloashiria amani baina yao na matarajio ni Ronaldo kusaini mkataba mpya siku chache zijazo. Perez alishaahidi kufanya atakavyoweza ili Ronaldo abaki Madrid, ikizingatiwa pia, mwezi uliopita wakati anachaguliwa kwa mara ya pili kuwa Rais wa klabu hiyo, Perez aliahidi kumbakiza mchezaji huyu mbele ya bodi ya klabu. Ronaldo amehusishwa kurudi Man utd au kwenda PSG, lakini hadi sasa inaonekana mchezaji huyu ataendelea kuwepo Madrid.  
Perez pia alikutana na makocha wa klabu hiyo Ancelotti na Zidane, ambao wote kwa pamoja wapo kwenye mkakati wa kufanya wawezalo kumbakiza Ronaldo. Leo Madrid watacheza mechi ya kwanza ya kirafiki na klabu ya AFC Bournemouth iliyopo daraja la pili nchini Uingereza. 

No comments:

Post a Comment