Wednesday, January 8, 2014

Azam, KCC, URA, Simba watinga nusu fainali


Azam FC 2 - 0 Cloves Stars 
URA 1 - 0 KMKM 
KCC* 0 - 0 Tusker (KCC 4 - 3 penati)
Simba 2 - 0 Chuoni 

Nusu fainali 

Azam FC vs KCC
URA vs Simba 

Mabingwa watetezi wa kombe la mapinduzi, Azam FC pamoja na timu mbili za Uganda; KCC na URA wamefanikiwa kutinga nusu fainali ya mashindano ya kombe la Mapinduzi yanayoendelea Zanzibar baada ya kuwabwaga wapinzani wao kwenye michezo ya robo fainali iliyopigwa leo Unguja na Pemba.

Katika mchezo ulipigwa saa nane mchana, Azam ilikuwa ya kwanza kutinga nne bora baada ya kuwabwaga Cloves Stars ya Pemba kwa magoli 2-0 yote yakifungwa kipindi cha pili na walinzi Aggrey Morris na Waziri Salaum.

Mchezo wa pili kwenye uwanja wa Gombani Pemba, watoza ushuru wa Uganda, URA wamewafyatua maafande/mabaharia KMKM kwa goli 1-0 la Owen Kasule dakika ya 42, sikisalia dakikatatu kabla ya mapumziko kwa mkwaju wa chinichini baada ya walinzi kuzembea kuondoa mpira langoni.

Kwenye mchezo wa Unguja KCC wamefanikiwa kucheza nusu fainali wakiwatoa mashindanoni makamu bingwa wa mwaka jana Tusker ya Kenya katika changamoto ya mikwaju ya penati baada ya dakika 90 kumalizika huku timu hizo zikiwa 0-0.

KCC walifaniukiwa kuweka kimiani penati zao zote 4 wakati Tusker wakifunga tatu tu na moja ya Ismail Dunga ikiokolewa na mlinda lango Salim Magoola na ya Luke Ochieng ikigonga mlingoti wa goli

Katika mchezo huo Tusker walilazimika kucheza dakika nne za mwisho wakiwa 10 baada ya kiungo Osborne Monday kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kuoneshwa kadi ya pili ya njano. 

Masuala mengine mawili muhimu ya mchezo huo ni la walinda milango wawili Ochieng na Magoola kupiga mikwaju yao ya penati kwa kufuatana na kufunga, na pia timu ya Tusker kumaliza dakika 90 bila kupiga hata mkwaju mmoja uliolenga lango huku KCC wakipiga mikwaju 5 langoni ambayo ama iliokolewa na kipa au kugonga mwamba.

Kwa matokeo hayo Azam itacheza na KCC katika nusu fainali ya kwanza huku URA wakicheza na Simba. Nusu fainali zote mbili zitachezwa Ijumaa hii na fainali ni Jumatatu Januari 13. Kwa niaba ya Azam TV

No comments:

Post a Comment