Wiki hii wapenzi wa soka duniani watashudia vigogo wa soka
Hispania na Ujerumani wanakutana katika nusu fainali ya klabu bingwa ulaya
(UEFA champions). Katika droo iliyofanyika tarehe 12/4/13, mchezo wa kwanza
utakuwa ni kati ya Bayern Munich vs Barcelona na mchezo wa pili utakuwa ni
Borussian Dortmund vs Real Madrid. Mashabiki wengi wa soka duniani walipenda kuona
timu za nchi moja hazikutani kwenye nusu fainali kitu ambacho kimekuwa kweli, ili
kujua ni nchi gani kati Ujerumani na Hispania wenye timu bora kwa sasa.
Uchambuzi wa MichezoUpdates unaonesha mwaka 2010 nchini
Afrika ya Kusini katika nusu fainali za kombe la dunia Ujerumani na Hispania
zilikutana katika mchezo mkali wenye upinzani ulioipa Hispania ushindi mfinyu
wa goli moja kwa bila, katika mechi hiyo asilimia 90 ya wachezaji waliocheza
kwa timu zote mbili Ujerumani na Hispania ndiyo waliopo hadi sasa kwenye vilabu
hivi vinne vinavyokutana katika michuano ya nusu fainali, hii inaonesha vita ya
Ujerumani na Hispania bado inaendelea na safari hii Wajerumani watahitaji
kuondoa uteja kwa Hispania. Matokeo ya FIFA yaliyotolewa mwezi huu yanaonesha
Hispania na Ujerumani bado wanafukuzana katika nafasi mbili za juu, Hispania
ikiwa ya kwanza na Ujerumani ya pili. Mambo haya mawili ni kielelezo cha kwanza
kinachoonesha utamu wa mechi hizi za nusu fainali UEFA champions.Kielelezo cha pili kinaonesha Bayern Munich na Barcelona
ndiyo timu zinazoongoza katika ligi za Ujerumani na Hispania zikiwa na tofauti
kubwa dhidi ya wapinzani wao walipo nafasi ya pili ambao ni Bourussia Dortmund
na Real Madrid. Hivyo kwa nusu fainali hii inawakutanisha washindi wa kwanza na
wapili kwenye ligi za Hispania na Ujerumani.
Wakati vuguvugu la nusu fainali likiwa limepamba moto kocha
wa Bayern Munich Heynckes amesema hana mpango wa kuomba ushauri kwa kocha wa
zamani wa Barcelona Pep Guardiola ambaye ameshasaini mkataba wa kuifundisha
Munich msimu ujao. Heynckes aliyasema hayo alipokuwa anaongea na jarida la
“Goal” baada ya kuulizwa kama atampigia simu Pep kumuomba ushauri, alisema
“naomba mniheshimu mimi na kazi yangu, siwezi kufanya kitendo kama hicho”.
Lakini ukweli halisi wa kauli hiyo hauwezi kujulikana kwasababu Pep anaijua
Barcelona nje ndani, na ni kweli atakuwa msaada mkubwa kwa benchi la ufundi la
Bayern kuweza kuwapa ushauri wa nini cha kufanya.
Mourinho kocha aliyeweza kushinda kombe la UEFA mara mbili akiwa
akiwa na timu tofauti ya Porto na Inter Milan, ataweka rekodi katika michuano
hii kama atafanikiwa kuiwezesha Real Madrid kuchukuwa ubignwa wa UEFA msimu
huu, akiweza kufanikisha hilo Mourinho atakuwa ni kocha wa kwanza kushinda
kombe hilo akiwa na timu tatu tofauti. Jose Mourinho ambaye anatarajiwa kurudi
Chelsea msimu ujao atahitaji kuondoka Real akiwa na rekodi nzuri ikiwa ni
pamoja na kushinda UEFA champions kombe ambalo Real wamelikosa kwa miaka kumi
na moja sasa. Borussia Dortmund ikiwa ni timu ambayo haijafika kwenye nusu fainali
kwa muda mrefu imefurahi kukutana tena na Real Madrid timu ambayo walikuwa wote
kwenye hatua ya makundi ambapo Dortmund waliweza kushinda 2-1 wakiwa nyumbani
na kutoka droo ya 2-2 Santiago matokeo ambayo yaliifanya Dortmund iongoze
katika kundi hilo la kifo lililojumuisha mabingwa wa England (Man city), Spain
(Real Madrid) na Holland (Ajax).
Barcelona timu ambayo inachukuliwa kuwa ndiyo timu bora duniani
imekuwa na presha kubwa ya kurudisha hadhi yake toka mwaka 2011 iliposhinda
kombe hili mara ya mwisho chini ya Pep Guardiola. Kumekuwa na fikra tofauti
kuwa Barcelona imeishiwa baada ya Pep kuondoka na wengine wakisema muda wao wa
kutamba umekwisha licha ya kuendelea kuwa tishio kwa timu pinzani lakini wao
Barcelona wanaamini timu yao ni kama zingine hivyo inaweza kushinda au kufungwa
licha ya kuwa mwaka huu wanauchukulia kama ni wao ikiwa ni kumbukumbu ya kurudi
tena Wembley kwenye uwanja walioshinda kombe hili kwa mara ya mwisho 2011.
Kocha wa Barcelona amekuwa nje ya uwanja kwa kipindi akitibiwa kansa kitu
ambacho kiliwaathiri Barca kwa kiasi kikubwa na kupelekea kupata matokeo mabaya
katika baada ya mechi, hali ya kuugua na kupata nafuu kwa kocha wao kumewafanya
wachezaji wajiunge kwa pamoja na kuweka ahadi ya kujitahidi kufa na kupona ili
wampatie zawadi ya kombe hilo Tito Vilanova kama ambavyo walivyofanya kwa Eric
Abdial mwaka 2011.
Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Robert Lewandowski na
Thomas Muller ni majina ambayo tunategemea kuyasikia zaidi katika nusu fainali
wakiwa ndiyo wachezaji tegemezi kwa timu hizi nne. Wachezaji hawa pamoja na
wengine muhimu wameonekana kupumzishwa kwenye michezo ya ligi kungojea siku ya
tarehe 23 na 24 April ambapo nusu fainali ya kwanza itachezwa jijini Munich na
Durtmund nchini Ujerumani.
Washibiki wengi duniani wamekuwa na fikra za kuona Clasico kwenye
fainali yani Barcelona vs Real Madrid ikiwa ni timu zenye upinzani mkubwa na
zinacheza mpira unaovutia, lakini kutimia hayo ni baada ya Real Madrid kumaliza
shughuli pevu kuwatoa Dortmund timu ambayo ilishawapa kichapo cha goli 2-1,
wakati Barcelona wao watatakiwa kuomba Messi, Xavi,Busquets na Iniesta wawe
kwenye fomu ya uhakika ili waweze kuvunja ngome ya ‘The Bavarians’ ili kufika
fainali.
No comments:
Post a Comment