Kansela Angela Merkel
amefadhaishwa na kashfa ya kukwepa kodi inayomkabili rais wa timu ya mpira wa
miguu ya Bayern Munich, Uli Hoeness. Kwa mujibu wa msemaji wa kansela
Seibert, Kansela Merkel amefadhaishwa sana na jambo hili kutokana na ukweli
kwamba Hoeness amekuwa kielelezo chema kwa Ujerumani, kwani sio tu kwamba
anaongoza klabu bora kabisa ya mpira, bali pia amekuwa akiunga mkono jithada
kadhaa za maendeleo, ukiwemo mradi wa kuwajumuisha wageni kwenye jamii ya
Ujerumani. Jambo hili ambalo limesharipotiwa kwenye vyombo vya dola kwa
uchunguzi zaidi mwendesha mashitaka Mkuu wa Munich, Ken Heidenreich,
amethibitisha kuendelea kwa uchunguzi dhidi ya Höness, ingawa hakutaja kiwango
cha fedha kinachohusika wala muda ambao uchunguzi huo utachukua.Hata hivyo,
Hoeness, mwenye umri wa miaka 61, amesema hana mpango wowote wa kujiuzulu
kutokana na tuhuma hizo za kukwepa kodi.
Badala yake, rais huyo wa Bayern
Munich, ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya timu hiyo, ameliambia gazeti la
Sport Bild Plus, atahudhuria kweye mechi ya nusu fainali ya Champions League
kati ya timu yake na Barcelona hapo kesho. Mwenyewe Hoeness, ambaye pia ni
mmiliki mwenza wa kiwanda cha kusindikia nyama, amekataa kuingia undani wa
suala hili, lakini ameahidi kutoa ushirikiano wowote unaohitajika kwa waendesha
mashitaka.
Ripoti hizo za kukwepa kodi ndizo
zilizohanikiza kwenye vyombo vya habari nchini Ujerumani na Hoeness amenukuliwa
na gazeti la Münchener Merkur, kwamba atajitetea kisheria dhidi ya vyombo vya
habari viinavyomtuhumu.
Höness, ambaye mwenyewe ni
mchezaji wa zamani wa Ujerumani ya Magharibi, amekuwa msemaji mkubwa kwenye
soka ya Ujerumani, Bundesliga. Alikuwa meneja wa kwanza kijana kabisa kwenye
Bundesliga, baada ya kuchukua nafasi hiyo akiwa na miaka 27 tu, kufuatia jeraha
lililohitimisha uchezaji wake uwanjani.
Baada ya zaidi ya miaka 30 akiwa
kama meneja wa kibiashara wa Bayern Munich, mwaka 2009 alimrithi Franz
Beckenbauer kama rais wa timu hiyo. Chini ya uongozi wake, klabu hiyo imekuwa
na mafanikio zaidi kuliko klabu zote za mpira nchini Ujerumnai na moja ya klabu
tajiri kabisa duniani. Habari hizi ni kwa mujibu wa DW
No comments:
Post a Comment