Klabu ya Yanga na Kocha Msaidizi
wa timu ya Toto Africans, Athuman Bilali wamepigwa faini ya sh. 500,000 kila
mmoja kutokana na makosa mbalimbali katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL)
inayoendelea nchini. Adhabu hizo zimetolewa na Kamati ya Ligi ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana Jumapili (Aprili 7
mwaka huu) jijini Dar es Salaam kupitia ripoti za waamuzi na makamishna kwa michezo
namba 108 hadi 171. Yanga imepigwa faini hiyo baada ya kupata kadi tano za
njano katika mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa Februari 7 mwaka huu.
Vilevile Kagera Sugar imepigwa faini ya sh. 100,000 kwa kuchelewa kufika kwenye
kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) dhidi ya African Lyon
iliyochezwa mjini Bukoba, Februari 23 mwaka huu. Naye Kocha Bilali
amepigwa faini hiyo na kufungiwa mechi tatu za ligi hiyo kwa kumshambulia kwa
maneno kocha wa timu pinzani, hali iliyosababisha mwamuzi amtoe kwenye benchi
la wachezaji. Alifanya tukio hilo kwenye mechi kati ya Toto Africans na
Tanzania Prisons iliyochezwa Aprili 3 mwaka huu jijini Mwanza.
No comments:
Post a Comment