Thursday, April 4, 2013

TFF Yazindua Mpango Wa Maendeleo 2013-2016


Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limezindua rasmi Mpango wa Maendeleo wa Mpira wa Miguu (Technical Development Plan- TDP) wa 2013-2016 ambao pamoja na mambo mengine unahusisha kutazama upya mfumo wa mashindano na kuunda kanda kwa ajili ya kusimamia maendeleo. Uzinduzi huo umefanywa leo (Aprili 4 mwaka huu) na Rais wa TFF, Leodegar Tenga katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na washirika mbalimbali wakiwemo wachezaji, viongozi wa mpira wa miguu, Serikali, klabu na Wahariri wa Michezo. 
Rais Tenga amesema mpango huo unafuatia ule wa 2004-2007, na 2008-2012 ambayo ilitengenezwa kwa msaada wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA). Mpango wa sasa umetengenezwa na TFF kwa kufuata mpango mfano (standard plan) wa FIFA. Amesema mpango wa sasa ni wa kiufundi zaidi kwa vile umelenga kuendeleza mpira wa miguu, kwani iliyotangulia ilihusisha zaidi kutengeneza muundo wa TFF, kazi ambayo imekamilika kwani sasa shirikisho lina vyombo mbalimbali vya kusimamia mchezo huo.
Tenga amewaomba wadau wote wa soka Tanzania kushirikiana ili kufanikisha mpango huu na amewashukuru wote waliotoa maoni kwa ajili ya mpango huo wenye kurasa 76. Mpango huo ulioandaliwa na Mkufunzi wa FIFA, Henry Tandau, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni na Ofisa Maendeleo wa TFF, Salum Madadi unapatikana kwenye CD na nakala laini (soft copy).

No comments:

Post a Comment