Kocha msaidizi wa timu ya Taifa (Taifa Stars) Sylvester Marsh amewapa moyo Watanzania kufuatia mchezo wa jumapili kati ya Taifa Stars na Ivory Coast utakaofanyika katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kuwania kufuzu kombe la dunia. Marsh ametoa kauli hiyo kufuatia hali ya unyonge iliyoanza kujitokeza kwa baadhi ya Watanzania kufuatia uwezo wa hali ya juu wa timu ya Ivory Coast, timu ambayo ni ya kwanza kwa ubora wa soka barani Afrika. Marsh alisema ' Nawaomba Watanzania wenzangu msiwe na wasiwasi wowote kwani timu yetu ni imara na haina sababu zozote za kupoteza mchezo wa jumapili, tumejiandaa vya kutosha na kikosi kipo tayari kuwakabili Ivory Coast'. Vilevile Marsh aliongelea masuala ya kiufundi ambapo aliwatoa hofu pia Watanzania kufuatia kukosekana kwa baadhi ya wachezaji akiwemo Bocco ambaye ni majeruhi na Morris aliyepewa kadi nyekundu kwenye mechi ya Morocco, Marsh alisema ' kukosekana kwa wachezaji hao sio tatizo kwa timu ya Tanzania kwani kikosi chetu kina wachezaji wengi wenye uwezo wa kuiwakilisha Tanzania, pia kwasasa tunatumia mfumo wa 4-4-1-1 ambao utakuwa rahisi kwa timu yetu kushambulia na kuzuia kwa nguvu zaidi'. Wakati huo huo, kocha mkuu wa Taifa Stars Kim Poulsen amewaasa Watanzania kutoangalia takwimu na matokeo yaliyopita bali waangalie kiwango na ari ya timu ili kujua mwenendo wa timu kwani takwimu wakati mwingine zinaweza kukatisha tamaa mahali penye uwezekano wa kufanikiwa. Taifa Stars inatarajiwa kushuka dimbani siku ya jumapili kucheza na Ivory Coast mchezo ambao Taifa Stars inatakiwa kushinda ili kurudisha matumaini ya kushiriki kwenye michuano ya kombe la dunia nchini Brazil mwakani.
Ifuatayo ni msimamo wa kundi la Tanzania hadi sasa
Team | MP | W | D | L | GF | GA | Pts |
---|---|---|---|---|---|---|---|
Ivory Coast | 4 | 3 | 1 | 0 | 10 | 2 | 10 |
Tanzania | 4 | 2 | 0 | 2 | 6 | 6 | 6 |
Morocco | 4 | 1 | 2 | 1 | 6 | 7 | 5 |
Gambia | 4 | 0 | 1 | 3 | 2 | 9 | 1 |
No comments:
Post a Comment