Klabu ya PSG ya Ufaransa imesema ipo tayari kulipa kiasi cha paundi mil 17 ili kumsajili kiungo mchezeshaji wa Newcastle, Yohan Cabaye. PSG imekuwa ikimnyemelea mchezaji huyu tokea dirisha dogo lifunguliwe, lakini hadi sasa klabu ya Newcastle imekuwa ikiweka ngumu kwa mchezaji huyu.
DailyMail linasema klabu ya Arsenal imefikia hatua nzuri ya mazungumzo na klabu ya Schalke ili kumsajili Julian Draxler. Mazungumzo baina ya klabu hizi mbili yamekuwa marefu kutokana na mahitaji ya paundi mil 35 kwa klabu ya Schalke ili kumruhusu Draxler kujiunga na Arsenal. Taarifa za DailyMail zinasema klabu ya Arsenal ipo tayari kutoa dau la paundi mil 30 ambazo ni pungufu ya paundi mil 5 jambo ambalo linaendelea kuchelewesha makubaliano. Licha ya chelewa chelewa iliyopo, klabu ya Arsenal boda ina uhakika mkubwa wa kumsajili mshambuliaji huyu kwani mchezaji mwenyewe na wakala wake wameshakubaliana na Arsenal.
Mbali ya kutangazwa na vyombo vingi vya habari kuwa Michael Essien ameshajiunga na klabu ya Ac Milan kwa mkopo, lakini kuna dosari zimejitokeza kuhusu usajili huu. Dosari yenyewe ni kuwa Essien ameonekana kuwa na majeraha kwenye kifundo cha mguu, jeraha ambalo lilimfanya akae nje ya uwanja kwa muda mrefu akiwa na Chelsea mwaka 2011. Jeraha hili ndilo lilifanya kiwango cha Essien kushuka na hata kumpoteza kwenye ramani ya viungo bora wa dunia. Klabu ya Ac Milan imesema itaangalia kwa undani majeraha hayo kabla ya kukubaliana na mchezaji huyu ila ikishindikana itabidi usajili wake usitishwe.
Kocha wa Man utd, David Moyes akiwa jijini Munich Ujerumani pamoja na Sascha Breese ambaye ni wakala wa Toni Kroos, Mario Gotze na Marco Reus. Moyes alitajwa kwenda jijini Munich kumuangalia Dante, lakini taarifa zilibadilika baada ya Moyes kuonekana na Sascha ambaye ni wakala wa wachezaji wengine waliotajwa. Kutokana na ziara hii ya Moyes, fununu zilizopo ni kwamba Moyes anafikiria kutuma maombi kwa Bayern Munich ili kumsajili Toni Kroos ambaye anacheza nafasi ya kiungo. Kama United watafanikiwa kumpata Kroos akisaidiana na Mata kwenye nafasi ya kiungo, basi hakika United watakuwa wamemaliza matatizo ya kiungo na kuna uwezekano mkubwa timu ikarudi kwenye kiwango chake kilichozoeleka.
Tayari klabu ya Chelsea imefikia makubaliano ya awali na klabu ya Atl. Madrid kumsajili mshambuliaji wa klabu hiyo Diego Costa mwishoni mwa msimu (mwezi Julai). Taarifa za Marca zinasema, klabu ya Chelsea italipa kiasi cha paundi mil 32 ili kumsajili Costa. Mbali ya Costa, klabu ya Chelsea pia imetajwa kuwa kwenye mazungumzo na klabu ya PSG ili kumsajili mshambuaji wa klabu hiyo Cavani kwa kulipa kiasi cha fedha pamoja na kuwapa Lukaku, dili hili linatarajiwa pia kufanyika mwishoni mwa msimu kama Atl. Madrid wataweka ngumu kumuachia Diego Costa.
Winga wa Man utd, Wilfried Zaha amewasili St. Georges Park kwenye jiji la Cardiff tayari kufanyiwa vipimo na hatimaye kujiunga na klabu ya Cardiff City, akiwa kama mchezaji wa mkopo hadi mwisho wa msimu huu.
The Sunday Times, gazeti la kila Jumapili nchini Uingereza linasema kuwa, kocha wa klabu ya Liverpool, Brendan Rodgers anamhitaji kiungo wa Benfica, Andre Gomes. Taarifa hizi zinasema Gomes anahitajika na Liverpool sio tu kuziba pengo la majeruhi Lucas Leiva ila pia ataandaliwa kuwa mrithi wa Steven Gerrard ambaye muda wake wa kucheza soka unakwenda ukingoni. Klabu ya Benfica imesema kuwa inahitaji kiasi cha paundi mil 12.7 kwa kinda huyu mwenye miaka 20 kujiunga na Liverpool. Taarifa zaidi ya usajili wa mchezaji huyu zitaendelea kutoka kwani Gomes ndiye ameonekana mchezaji mbadala kwa klabu ya Liverpool baada ya kumkosa Salah aliyejiunga Chelsea.
No comments:
Post a Comment