Dailysport limewataja wachezaji hawa pichani kuwa kwenye orodha ya watakaomwagwa na United mwishoni mwa msimu huu. Wachezaji hao ni pamoja na Patrice Evra, Nemanja Vidic, Rio Ferdinand, Ryan Giggs, Anderson, Alex Buttner, Nani, Ashley Young, Shinji Kagawa na Tom Cleverley. Sababu mbalimbali zimetajwa kusababisa wachezaji hawa kumwagwa ikiwa ni pamoja na umri mkubwa, kiwango kidogo na kushindwa kuoana na mfumo wa Moyes. Nemanja Vidic yeye imeshajulikana kuwa atajiunga na klabu ya Inter Milan na ameshasaini mkataba na timu hiyo. Ryan Giggs ambaye ni kocha msaidizi wa United anatarajiwa kuachana na kucheza soka ili abakie kuwa kocha msaidizi, kwani umri wake umeshakwenda mno.
Wachezaji wengine ambao umri wao unawafanya waondoke United ni pamoja na Rio mwenye miaka 35 na Evra miaka 32, ambapo habari zinasema Evra anaweza kujiunga na klabu ya Monaco ya Ufaransa mwishoni mwa msimu huu. Nani yeye anaweza kurudi Ureno klabu ya Porto ambayo ilikuwa ikimuhitaji tokea msimu uliyopita. Nani mwenyewe alishaonesha nia ya kutaka kurudi Ureno, hivyo jambo hili linaweza kuwa jepesi kwa Moyes kumruhusu aondoke, vilevile kwa Anderson ambaye yupo nchini Italia akichezea Fiorentina kwa mkopo. Kwa upande wa Kagawa, bado kuna mjadala mkubwa ndani ya klabu kwa viongozi na washabiki, kwani kuna upande unaokubali Kagawa arudi Ujerumani, Dortmund, lakini kuna upande mwingine unasema mchezaji huyu aendelee kubaki United kwani ana kiwango kizuri ila bado hajapata muda wa kutosha wa kucheza tokea asajiliwe. Uamuzi wa mwisho kuhusu Kagawa utabakiwa kwa kocha Moyes licha ya kuwa dalili kubwa inaonesha ataweza kumruhusu aondoke kwani hadi sasa amempanga mara 14 kati ya mechi 33 za ligi ambazo United imeshacheza hadi sasa.
Buttner, Young na Cleverley walikuwa wachezaji wazuri sana wakati wa Sir Alex Ferguson, lakini msimu huu viwango vyao vimeshuka ghafla jambo ambalo linamfanya Moyes awe na kigugumizi cha kuwabakiza United na kuendelea kuongeza mzigo wa kuwalipa mishahara. Wachezaji hawa watatu wanaweza kutolewa kwa mkopo ili waendelee kuangaliwa na kuongeza viwango vyao. Uamuzi huu mkubwa wa kusafisha klabu unaotarajiwa kufanywa na Moyes una lengo la kuimarisha timu ili kurudisha hadhi ya United ambayo msimu huu imekuwa ni njia ya kupata pointi tatu kwa timu nyingi. Wachezaji ambao wameshatajwa kujiunga na United kuziba mapengo ya wachezaji hawa ni pamoja na Toni Kroos (Bayern Munich), William Carvalho (Sporting Lisbon), Luke Shaw (Southampton), Eliaquim Mangala (Porto), Pjanic (Roma) na Koke (Atl. Madrid) na wengine. Jumla ya paundi mil 200 imetengwa kwa ajili ya Moyes kufanya usajili mwishoni wa msimu huu.
No comments:
Post a Comment