Friday, May 10, 2013

Brandts awahakikishia Yanga ushindi

Kocha wa klabu ya Yanga, Brandts amesema nguvu zote kwasasa ameelekeza kwenye mechi yao dhidi ya Simba na anaamini watashinda ili kuendeleza furaha kwa wanajangwani. Mechi hiyo itakayofanyika tarehe 18 Mei kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam inamuumiza kichwa kocha wa Yanga kwasababu ni mechi ya upinzani na kama Yanga wakifungwa hata furaha ya kutwaa ubingwa itapungua. Katika maneno yake Brandts alisema "Mchezo wa mwisho kwetu ni fainali kwa sababu tunahitaji kuendeleza ushindi, tumefanya hivyo katika michezo 12 ya awali tuliyocheza na waaamini vijana wangu wako vizuri kuelekea mchezo huo ambao naamini tutaibuka na ushindi na kusherekea ubingwa vizuri pamoja na mashabiki, viongozi na wanachama watakaokuwa wamejitokeza katika dimba la uwanja wa Taifa". Mbali na hayo Brandts pia alitoa maneno yake ya shukrani kwa wachezaji, uongozi wa timu pamoja na mashabiki wa Yanga kwa umoja wao waliounesha katika kipindi chote cha ligi na kusema umoja huo ndiyo chachu ya mafanikio na ushindi kwa wanajangwani. Wakati huo huo timu ya Yanga leo imeendelea na mazoezi ya nguvu kujiandaa na mchezo wake unaofuata dhidi ya Simba.

No comments:

Post a Comment