Thursday, May 16, 2013

FIFA kigugumizi kuhusu kombe la dunia 2022

Shirikisho la mpira wa miguu duniani FIFA bado lipo kwenye kigugumizi kuhusiana na miezi itakayotumika kufanya kombe la dunia la mwaka 2022 nchini Qatar. Kigugumizi cha FIFA kinakuja kutokana na hali ya joto la nchi ya Qatar kipindi cha mwezi wa watano hadi wa saba miezi ambayo kombe la dunia huwa linafanyika. Nchi ya Qatar huwa ina joto linalofikia digrii 50 kuanzia mwezi wa tano hadi wa saba kitu ambacho kitaadhiri michuano hiyo. Mwezi uliopita nchi ya Qatar ilithibitsha kuwa hakutakuwa na tatizo lolote kuhusiana na jambo hilo kwani wameshapata teknolojia ya kupooza joto kwenye viwanja lakini wadau wengi wa soka wamepinga kauli hiyo ya Qatar wakisema teknolojia hiyo itaweza kupoza joto ndani tu ya viwanja lakini nje kutakuwa na joto. Wadau wamehoji swala hili kwasababu kombe la dunia linaambatana na vitu vingi ikiwemo michezo mbalimbali nje ya viwanja na mitaani kitu ambacho kitawaadhiri sana mashabiki. Vilevile, timu nyingi zinapendelea kufanya mazoezi kwenye viwanja vya wazi ambavyo haiwezekani kuweka viyoyozi hali ambayo itazifanya timu zote kufanya mazoezi kwenye viwanja vya ndani. Kutokana na hali hii baadhi ya wadau wa soka wakiwemo baadhi ya viongozi wa FIFA wamependekeza michuano hiyo ifanyike mwezi novemba na disemba kitu ambacho kitaadhiri michuano ya ligi mbalimbali duniani ambayo hufanyika kuanzia mwezi wa nane hadi wa tano. Hali hii ndiyo inaifanya FIFA hadi leo ibakie na kigugumizi cha kuamua kama kombe la dunia litafanyika kwenye miezi ya kawaida au itabadilishwa. Sepp Blatter raisi wa FIFA yeye ameendelea kusimama na msimamo wake kuwa michuano hiyo itafanyika miezi ile ile (wa tano hadi wa saba) lakini msimamo wake unakuja ili kulinda maamuzi ya kamati kuu ya FIFA iliyotoa uamuzi michuano hiyo ifanyika Qatar, uamuzi ambao umeonekana kuwa na dosari. Midahalo na vikao vingi vimeshafanyika kujadili swala hili lakini hadi leo jibu halijapatika, lakini jibu lazima lipatikane kwasababu michuano hiyo lazima itafanyika. 

No comments:

Post a Comment