Mchezaji wa Washington Wizards Jason Collins ametangaza
rasmi kuwa yeye ni shoga baada ya uvumi wa muda mrefu. Jason alijitangaza kwenye jarida la Sports Illustrated lililomnukuu akisema ‘Mimi
nina umri wa miaka 34, mchezaji mweusi wa NBA ni shoga’, taarifa hizi
zimelipuka kwenye vyombo vya habari nchini Marekani kwani sio jambo la kawaida
kwa mchezaji wa NBA kujitangaza hadharani kuhusu ushoga. Jason katika mahojiano
na ABC News leo asubuhi amesema, baada ya kujitangaza hadharani anajisikia kuwa
huru na mwenye furaha sana. Kufuatia kauli hiyo ya kujiweka hadharani, watu
wengi maarufu nchini Marekani akiwemo
rais mstaafu Bill Clinton na mchezaji mwenzake Kobe Bryant wamempongeza Jason kwa
uamuzi wake na wametoa ombi kwa wachezaji wengine kufuata nyayo za Jason. Lakini
uchambuzi umeonesha kuwa licha ya Marekani kuwa mbele kimaendeleo ya jamii
hususani uhuru wa kuongea na kudumisha haki za binadamu lakini bado itakuwa
vigumu kwa wachezaji wote ambao ni mashoga kujitangaza kwasababu wanahofia
kubaguliwa, kuzomewa na hata kukosa huduma zingine kama mashoga. Nchi nyingi
barani Ulaya na Amerika zimekuwa zikihamasisha kukubalika kwa ushoga ikiwa ni sera
za kisiasa ili kushinda chaguzi mbalimbali lakini ndani ya jamii zenyewe za wa
Amerika na Ulaya bado jambo hili la ushoga halijakubalika katika jamii yote.
Vilevile, jamii kubwa inachukulia mtu shoga kama ni dhaifu hivyo kwa
wanamichezo ambao wanatakiwa kuwa wakakamavu itakuwa vigumu sana kujitangaza kuwa ni mashoga kwani ajira zao zinaweza kuzorota na pia kupoteza mashabiki.
Jason Collins mwenye urefu wa futi 7 kabla ya kujiunga na Washington Wizards mwaka
huu ameshacheza kwenye timu kubwa za NBA zikiwemo Boston Celtics, Atlanta
Hawks, Memphis Grizzlies, Minnesota na New Jersey Nets.
No comments:
Post a Comment