Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Naibu Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni Mh Amos Makalla imezitoa kibali rasmi kwa klabu za Simba, Yanga na Falcon ya Zanzibar kushiriki kwenye michuano ya Kagame Cup nchini Sudan mwaka huu. Wakati taarifa hizo zinatoka tayari shirikisho la mpira wa miguu Afrika Mashariki Cecafa lilishachagua timu za URA, Elite Sports na Rayon sports kuchukua nafasi za timu za Tanzania ambazo hadi jana zilikuwa zimeshatangaza kujitoa kwenye michuano hiyo kutokana na hofu ya kiusalama nchini humo. Akielezea jambo hili, Mh Makalla alisema kama serikali walikuwa wanangojea taarifa za kimaandishi kutoka kwa serikali ya Sudan kuzihakikishia timu za Tanzania usalama wao. Lakini taarifa hizo za kimaandishi kutoka kwa serikali ya Sudan zimechelewa kufika jambo ambalo limesababisha klabu za Tanzania kuenguliwa kwenye michuano hiyo. Klabu ya Yanga ndiyo imeathirika zaidi kwani ilikuwa ni bingwa mtetezi wa michuano hiyo, hivyo imeweza kuachia kombe bila ya kulipigania. Michuano hiyo ya Kagame inatarajiwa kuanza jumanne ijayo ya tarehe 18 hadi Julai 2 nchini Sudan.
No comments:
Post a Comment