Baada ya klabu ya Man utd kufanya vibaya katika ligi kwa kufungwa mechi tatu kati ya sita na kucheza mchezo mbovu tofauti na ilivyozoeleka, baadhi ya kasoro zimeanza kuonekana waziwazi ambazo kwa kiasi kikubwa zimechangiwa na David Moyes ambaye ni kocha mpya wa Man utd. Kasoro hizi ni kama zifuatazo;
1. Moyes aliwatema wasaidizi wa Sir Alex Ferguson
Kwenye picha ni Mike Phelan (kushoto) na Rene Meulensteen (kulia), hawa walikuwa wasaidizi wakuu wa Sir Alex Ferguson. Taarifa zinasema, baada ya Sir Alex kumchagua Moyes kuwa kocha mpya wa United, alimshauri kuendelea na wasaidizi hawa, kwani watamsaidia kwenye mambo mengi ya kiufundi, lakini Moyes alipingana na mapendekezo ya Sir Alex na kuja na timu mpya ya wasaidizi wake akiwemo Steve Round, Jimmy Lumsden, Chris Woods na Phil Neville. Jambo hili limekuwa ni moja sababu kubwa inayo sababisha kudorora kwa Man utd, kwani benchi lote la ufundi limeundwa na watu ambao hawana uzoefu wa muda mrefu kwenye kazi hiyo wakiwa na Man utd.
Picha ya juu ni Sir Alex akiwa na wasaidizi wake na picha ya chini ni Moyes akiwa na wasaidizi wake |
2. Kushindwa kusajili kiungo mshambuliaji
Sababu ya pili ambayo imechangia klabu ya Man utd kuanza vibaya msimu huu wa ligi ni kushindwa kufanya usajili wa kiungo mshambuliaji kwenye kipindi chote cha usajili. Majina kadhaa ya viungo washambuliaji yalitajwa kuhusika na usajili wa kwenda United, lakini hadi dirisha la usajili linafungwa Man utd ilishindwa kusajili mchezaji yoyote kwenye nafasi hiyo. Baadhi ya wachezaji ambao walitajwa kusajiliwa na United ni Cesc Fabregas, Thiago Alcantara, Modric n.k. Sababu kubwa ya kushindwa kumsajili mchezaji yoyote mwenye uzoefu kati ya hawa ilitajwa ni David Moyes ambaye alishindwa kushauriana na CEO, Ed Woodward. Matokeo yake United iliamua kumsajili Fellaini mchezaji ambaye hana uwezo wa kujenga mashambulizi kama ilivyokuwa kwa Paul Scholes, hali ambayo imesababisha Man utd kucheza hovyo kwenye safu ya kiungo.
3. Kuwaweka benchi baadhi ya wachezaji wenye uwezo
David Moyes ameonekana kutojua vyema uwezo wa baadhi ya wachezaji ambao anaweza kuwatumia kwenye mechi tofauti. Sababu hii imekuja kutokana na ukweli kwamba klabu ya Man utd ina wachezaji zaidi ya wawili kwenye kila nafasi ambao wana uwezo wa kucheza kiwango kinachokaribiana, lakini tokea ligi ianze Moyes hajaweza kuwatambua baadhi ya wachezaji ambao wangeweza kucheza vizuri kwenye nafasi ambazo zimeonekana kuwa dhaifu. Baadhi ya wachezaji ambao Moyes hajawapa nafasi ya kutosha kwenye kikosi chake cha kwanza ni Kagawa, Nani, Phil Jones na Evans wachezaji ambao wangeweza kubadilisha kwa kiasi kikubwa aina ya uchezaji wa Man utd.
Sababu hizi tatu ndizo zimeonekana waziwazi kuchangia mwenendo mbovu wa klabu ya Man utd tokea Sir Alex Ferguson aondoke. Msimu uliopita Man utd ilicheza mechi 38 na ilifungwa mechi tano tu, lakini msimu huu Man utd imeshacheza mechi sita na imefungwa mechi tatu. Hali hii inaonesha Man utd itafungwa zaidi ya mechi tano kwenye msimu huu jambo ambalo linaweza kupelekea kukosa ubingwa na kupigana kwa mbinde kupata nafasi ya kucheza klabu bingwa Ulaya.
No comments:
Post a Comment