Saturday, April 13, 2013

Yanga yaivua ubingwa Simba, imeshinda 3 - 0

Mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara Simba Sports Club ya jijini Dar es salaam leo imevuliwa rasmi ubingwa baada ya Yanga kushinda magoli 3-0 dhidi ya JKT Oljoro katika mchezo uliyofanyika kwenye uwanja wa taifa jiji Dar es salaam. Simba imevuliwa ubingwa huo baada ya Yanga kufikisha pointi 52, pointi ambazo Simba haiwezi kuzifikisha hata ikishinda michezo yote iliyobaki. Simba yenye pointi 35, imebakiza michezo mitano, kama itashinda michezo yote mitano itafikisha pointi 50 ambazo hazitatosha kuifikia Yanga. Simba itashuka dimbani kesho kupambana na Azam FC katika mchezo wenye ushindani mkubwa wa kugombea nafasi ya pili. Azam FC ina pointi 46 inahitaji kushinda mchezo wa kesho ili kuendeleza matumaini ya kuchukua ubingwa. Katika mchezo wa leo Yanga walianza mpira kwa kasi nakuweza kujipatia goli la kwanza dk ya tano kupitia beki wake kati Cannavaro, wakati magoli mengine yakifungwa na Msuva dk ya 20 na Kiiza akifunga dk ya 43. Kwa ushindi huu Yanga imefikisha pointi 52 tofauti ya pointi sita dhidi ya Azam FC yenye pointi 46, hivyo Yanga inaombea Azam FC afungwe na Simba kitu ambacho kinatokea kwa mara ya kwanza katika soka la Tanzania kwa mpinzani wa jadi kumtakia mema mwenzake. 

No comments:

Post a Comment