Saturday, May 18, 2013

Azam Fc imeonesha mfano, ukiritimba wa Simba na Yanga umepata upinzani wa kweli

Ukiritimba wa Simba na Yanga umeonekana kuanza kupotea kwenye soka la bongo kadri siku zinavyozidi kwenda mbele. Mwaka jana tulishuhudia Simba na Azam FC wanawakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa wakati Yanga walikuwa wametupwa nje, lakini vilevile mwaka huu Yanga na Azam Fc watawakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa baada ya Yanga kushika nafasi ya kwanza na Azam Fc nafasi ya pili wakati Simba imetupwa nje ya michuano hiyo baada ya kushika nafasi ya tatu. Hali hii inaonesha kwa jinsi gani klabu ya Azam imeweza kushikilia nafasi ya pili kwa misimu mfululizo jambo ambalo linaleta matumaini kwa Watanzania kuwa soka limeanza kupanda. Lakini vilevile wiki hii kocha wa timu ya taifa Kim alitangaza kikosi cha taifa kitakachopambana na Morocco Juni 8, kwenye kikosi hicho tumeshuhudia Azam Fc inatoa wachezaji 9 wakati Simba na Yanga zikiwa na wachezaji 6. Jambo hili pia linaonesha kwa kiasi gani Usimba na Uyanga umeanza kupotea baada ya kuanza kupata upinzani unaostahiki. Kwa hali hii hakuna atakaye shangaa msimu/misimu ijao kuona Azam Fc inakuwa bingwa wa ligi kwani ni klabu pekee nchini ambayo imeweza kuleta mapinduzi ya kweli kwenye soka kwani mbali ya kuwa na wachezaji wakubwa pia imeweza kupiga hatua kwa kuwa na kiwanja chake yenyewe chenye vifaa na nyenzo mbalimbali za kisasa za kufanyia mazoezi lakini pia Azam Fc imefanikiwa kujenga mahusiano mazuri na vilabu vya nje jambo ambalo limewezesha baadhi ya wachezaji kufanya majaribio nje ya nchi na wengine kufanikiwa kujiunga na timu za nje. Maendeleo haya yamekuja kwasababu Azam ni timu binafsi na inaendeshwa kisasa, jambo ambalo linawafanya watu wote walioajiriwa kuwajibika. Maendeleo ya aina hii kwenye soka ndiyo Tanzania ilikuwa inayangojea kwa muda mrefu kwani ulimwenguni kote kwenye nchi ambazo zimeendelea kwa soka watu wengi binafsi wamewekeza kwenye soka na kuhamisha umiliki wa timu kutoka kwa wananchi kwenda kwenye miliki binafsi jambo ambalo limeweza kuleta mafanikio makubwa, hivyo uwekazaji wa namna hii ndiyo unatakiwa Tanzania ili kuweza kuinua zaidi soka letu. 


Mh. Raisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya M Kikwete akijaribu moja ya vifaa vya Azam Fc siku ya ufunguzi wa uwanja wa Azam

No comments:

Post a Comment