Friday, May 17, 2013

Taifa Stars yawakosa Misri,Algeria & Libya kirafiki

Timu ya taifa Taifa stars mwezi Juni tarehe 8 inatarajiwa kucheza mechi yake ya marudio dhidi ya Morocco kwenye michuano ya kufuzu kombe la dunia. Katika kufanikisha ushindi wa mechi hiyo TFF ilikuwa imetoa maombi ya mechi za kirafiki kwa baadhi ya timu za Afrika kabla ya mchezo huo lakini mipango hiyo yote imeingia dosari. Awali TFF ilikuwa imeitafutia Taifa Stars mechi ya kirafiki Juni 1 mwaka huu dhidi ya Algeria, Libya au Misri. Lakini baadaye Algeria ikasema itacheza na Togo, wakati Misri ilitaka mechi hiyo ichezwe Juni 4 jijini Cairo, jambo ambalo lisingewezekana kwa Stars kwani ina mechi ya mashindano Juni 8 mwaka huu. Kwa upande wa Libya mechi hiyo ilikubaliwa ichezwe Tunis, Tunisia, Juni 2 mwaka huu. Lakini baadaye Libya ikataka mechi hiyo ichezewe jijini Tripoli ambapo TFF ilikataa kutokana na sababu za kiusalama. Licha ya mazingira haya Taifa stars imefanikiwa kupata mechi moja ya kirafiki dhidi ya Sudan itakayochezwa Juni 2 jijini Addis Ababa nchi Ethiopia kabla ya kwenda Morocco. Ikumbukwe mechi ya mwanzo kati ya Stars na Morocco, Taifa stars ilishinda magoli 3-1 jijini Dar es salaam. 

No comments:

Post a Comment