Monday, January 6, 2014

Tetesi za usajili leo tarehe 7 Jan 2014

Moyes
Wachezaji wanne wamethibitishwa na Dailysport kuwa mmoja wao ndiye atasajiliwa na Man utd kuziba pengo lililopo sasa kwenye nafasi ya kiungo. Wachezaji hawa wanne kama wanavyoonekana kwenye picha ni Fabregas, Gundogan, Reus na Shaw ambao hadi sasa wanafanya vizuri kwenye klabu zao na wametajwa kumridhisha Moyes kwa viwango vyao. Vilevile imeelezwa kuwa uongozi wa klabu ya Man utd utakutana na kocha Moyes wiki hii ili kuongea naye kuhusu mwenendo wa timu ikiwa pamoja na usajili wa dirisha dogo. Kikao hicho kinategemea kutoa majibu ya tetesi zilizopo hadi sasa kuhusu wachezaji mbalimbali wanaohusishwa na klabu ya Man utd.  

Klabu ya Arsenal imeendelea kuhusishwa na usajili wa mshambuliaji wa Bayern Munich, Mario Mandzukic. Tetesi za usajili wa mchezaji huyu kwenda Arsenal zimeongezeka baada ya klabu ya Bayern Munich kuthibitisha kumsajili mshambuliaji wa Dortmund R. Lewandowski. Taarifa kutoka kwenye gazeti la Marca zinasema klabu ya Arsenal imetenga kiasi cha Euro 25m kwa ajili ya kusajili mshambuliaji, fedha ambazo zimetajwa kukidhi bajeti ya kumsajili Mandzukic. 

Aliyekuwa kocha wa Tottenham Andre Villas-Boas ametajwa na vyombo mbalimbali vya habari kuwa anatarajiwa kuwa kocha mkuu wa klabu ya Ac Milan. AVB aliyefukuzwa na Tottenham baada ya kuboronga kuiongoza klabu hiyo anatarajiwa kujiunga na Ac Milan ili kuchukua nafasi ya Massimiliano Allegri ambaye ameonekana kushindwa kuiongoza klabu hiyo. Ac Milan kwasasa inashikilia nafasi ya 11 na imeshinda mechi 5 tu kati ya 18 ilizocheza. 

Goal UK linaripoti kuwa kiungo mshambuliaji wa Chelsea Juan Mata hawezi kuondoka ndani ya klabu hiyo ndani ya msimu huu. Goal limesema taarifa hizi zimethibitishwa na kocha wake Jose Mourinho akisema "Mata haondoki Chelsea kwa pesa yoyote hata kama anapata wakati mgumu kugombania nafasi dhidi ya Hazard, Oscar na Willian. 

Klabu ya Borussia Mönchengladbach imethibisha kuwa mlinda mlango wa kutegemewa Ter Stegen hatasaini mkataba mwingine na klabu hiyo ili kujiunga na Barcelona. Borussia Mon imesema Stegen alikuwa aongeze mkataba wake mwaka huu lakini amekataa kwani tayari ameshasaini mkataba wa makubaliano na klabu ya Barcelona. Barcelona wanatarajia kumsajili Stegen ili kuziba pengo la Valdes ambaye anamaliza mkataba wake mwisho wa msimu huu na anatarajia kujiunga na PSG au Monaco. 

Mshambuliaji wa zamani wa Chelsea Salomon Kalou anatarajiwa kurudi tena kwenye ligi ya England baada ya kuhusishwa na klabu ya Liverpool. Taarifa kutoka gazeti la The Mirror zinasema klabu ya Liverpool inaweza kumsajili Kalou ili aweze kuisaidia klabu hiyo kuziba mapengo ya wachezaji wanaopatwa na majeraha.

Taarifa kuhusu Mario Balotelli kurudi tena ligi kuu ya England zimeendelea kupamba vyombo vya habari nchini England na Italia vikihusisha mchezaji huyu kujiunga na Chelsea. Mahusiano mazuri kati ya Mourinho na Balotelli imetajwa kuwa sababu kubwa ya mchezaji huyu kujiunga na Chelsea. 

Espana linaripoti kuwa klabu ya Real Madrid imempatia ofa Fabio Coentrao kujiunga na Man utd kwa dau la paundi mil 12. Coentrao anatakiwa kutoa jibu la ofa hii ndani ya siku chache, ambapo wakala wake tayari ameanza kuifanyia kazi ofa hiyo. Coentrao alikuwa asajiliwe na Man utd mwaka jana, lakini usajili wake ulishindikana kwa sababu mbalimbali ikiwemo kushindwa kukubaliana baina ya klabu hizi mbili. Lakini sasa usajili huu unaonekana kuwa mwepesi, kwani kocha wa Madrid Carlo Ancelotti ameshamwambia Coentrao kuwa anaweza kuondoka muda wowote. 

Klabu za Man city na Liverpool zimehushwa kwa kiasi kikubwa kumsajili Xavi Alonso ambaye mkataba wake unatarajiwa kuisha ndani ya mwaka huu. Alonso ameshapewa mkataba mpya na Real Madrid, lakini ameonesha kukataa kuusaini na inasemekana anataka kuondoka Madrid na lengo lake kubwa ni kurudi kwenye ligi ya England. Klabu ya Liverpool ndiyo yenye nafasi kubwa ya kumsajili mchezaji huyu kutokana na mahusiano mazuri yaliyopo baina yake na klabu ikiwa sambamba na mapenzi ya washabiki wa Liverpool kumtaka arudi.

No comments:

Post a Comment