Thursday, February 20, 2014

Yanga yaendelea na mazoezi Bagamoyo kujiandaa na michezo ya ligi kuu

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara timu ya Young Africans wameendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo wake wa siku ya jumamosi dhidi ya Maafande wa Jeshi la Kujenga Taifa Ruvu Shooting ikiwa ni muendelezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu utakaofanyika katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam. Young Africans itacheza mchezo huo wa raundi ya 17 baada ya kuwa na michezo miwili ya Klabu Bingwa Barani Afrika dhidi ya timu ya Komorozine de Domoni kutoka visiwa vya Comoro ambapo waliitoa kwa jumla ya mabao 12-2 na kufuzu katika hatua ya pili.

Kikosi cha mholanzi Hans Van der Pluijm kimeingia kambini jana jioni katika Hoteli ya Kiromo mjini Bagamoyo kujiandaa na mchezo ambapo timu itakua ikifanya mazoezi mpaka itakaporejea siku ya jumamosi tayari kuwakabili maafande wa Ruvu Shooting. Jumla ya wachezaji 25 wameingia kambini mjini Bagamoyo kujiandaa na mchezo huo wa jumamosi ambapo itakua ni sehemu ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Al Ahly wiki ijayo katika mashindano ya Klabu Bingwa Barani Afrika. Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Young Africans iliweza kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting bao lililofungwa na mshambuliaji wa kimataifa kutoka nchini Uganda Hamis Kiiza.

No comments:

Post a Comment