Mwenyekiti wa klabu ya Simba Isamil Aden Rage amesema ni kweli viongozi wa vilabu vya Tanzania hawana malengo ya kushinda vikombe vya kimataifa ikiwemo michuano ya Afrika na Dunia. Rage ameyasema hayo kufatia kauli aliyoitoa mshambuliaji wa TP Mazembe Mbwana Samatta kuwa 'vilabu vikubwa vya Tanzania havina mipango ya kushinda vikombe vya Afrika, wao mipango yao ni kushinda kombe la ligi na kumfunga mpinzani wake'. Katika kuthibitisha hilo Rage amesema kauli ya Mbwana ni ya kweli ndiyo maana vilabu vya Tanzania hutolewa mapema kwenye michuano ya Afrika kwasababu havijajipanga kushindana kimataifa. Rage akiongelea vilabu vya Simba na Yanga ambavyo ndiyo vikubwa, alisema 'mipango ya Simba ni kumfunga Yanga na kuchukua ubingwa, hivyo hivyo kwa upande wa Yanga, kitu ambacho kitaendelea kutufanya tuishie hapa hapa miaka nenda rudi'. Mwaka huu Tanzania imewakilishwa na Simba, na Azam FC kwa upande wa Tanzania bara pamoja na Mafunzo na Super Falcon kwa upande wa Zanzibar, lakini hadi sasa Tanzania imebakiza timu moja tu ya Azam FC ambayo wiki hii itacheza na AS FAR ya Morocco katika mchezo ambao utakuwa mgumu kwa Azam baada ya kutoka droo ya bila kufungana jijini Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment