Friday, April 19, 2013

Ulinzi London Marathoni waimarishwa zaidi

Mbio za Jumapili Aprili 21 za marathon jijini London zinaandaliwa huku kukiwa na ulinzi mkali ulioimarishwa kufuatia mashambulizi ya bomu yaliyozikumba mbio za marathon za Boston nchini Marekani jumatatu ya wiki hii. Milipuko hiyo miwili ambayo iliwauwa watu watatu na kuwajeruhi wengi mjini Boston, imewalazimu waandalizi wa mbio za London kuimarisha mikakati ya usalama katika jitihada za kuwapa matumaini wanariadha pamoja na watazamaji wanaokadiriwa kufikia nusu milioni watakaojitokeza kushangilia mitaani. Mitaa yote itakayotumiwa katika mbio za Marathon za London imewekwa ulinzi mkali. Vilevile, Wanariadha watavaa vitambaa vyeusi kama kumbukumbu ya wale waliopoteza maisha katika mashambulizi ya Boston na waandalizi wamesema pia Euro mbili na senti thelathini zitatolewa na kila mwanariadha atakayemaliza mbio hizo kugharamia waathiriwa wa mashambulizi ya Boston.

No comments:

Post a Comment