Tuesday, April 9, 2013

TFF yatembeza faini kwa Yanga, Kagera na Kocha wa Toto

Klabu ya Yanga na Kocha Msaidizi wa timu ya Toto Africans, Athuman Bilali wamepigwa faini ya sh. 500,000 kila mmoja kutokana na makosa mbalimbali katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoendelea nchini. Adhabu hizo zimetolewa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana Jumapili (Aprili 7 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kupitia ripoti za waamuzi na makamishna kwa michezo namba 108 hadi 171. Yanga imepigwa faini hiyo baada ya kupata kadi tano za njano katika mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa Februari 7 mwaka huu. Vilevile Kagera Sugar imepigwa faini ya sh. 100,000 kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) dhidi ya African Lyon iliyochezwa mjini Bukoba, Februari 23 mwaka huu. Naye Kocha Bilali amepigwa faini hiyo na kufungiwa mechi tatu za ligi hiyo kwa kumshambulia kwa maneno kocha wa timu pinzani, hali iliyosababisha mwamuzi amtoe kwenye benchi la wachezaji. Alifanya tukio hilo kwenye mechi kati ya Toto Africans na Tanzania Prisons iliyochezwa Aprili 3 mwaka huu jijini Mwanza.

No comments:

Post a Comment