Thursday, May 23, 2013

Thiago aiweka Barca njia panda, anataka kwenda Man utd

Kiungo chipukizi wa Barcelona Thiago Alcantara msimu huu tena ameiweka njia panda klabu yake baada ya kuona ahadi alizopewa hazijatimia. Thiago anayetarajiwa kuchukua nafasi za kina Iniesta na Xavi ameonekana kukata tamaa ya kungojea lini atakuwa kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo jambo ambalo linampa kishawishi cha kuondoka Barcelona. Mwaka juzi Thiago aliomba kuondoka akihusishwa kuhamia Madrid au England lakini uongozi wa klabu hiyo ukiongozwa na Guardiola waliweza kumshawishi abakie wakampa ahadi ya kupata namba na vilevile wakampatia namba mpya ya jezi ambayo ndiyo namba anayoivaa hadi sasa 11. Lakini ahadi hizo zimeonekana kuwa feki kwa kiungo huyo kwani hadi sasa hayupo kwenye kikosi cha kwanza na haijajulikana lini Iniesta na Xavi watamuachia namba. Uongozi wa Barcelona unatambua msongo wa mawazo aliokuwa nao Thiago lakini wamekosa njia ya kufanya ili wamridhishe kwasababu Xavi na Iniesta bado wapo kwenye kiwango cha juu. 

Barcelona wapo kwenye njia panda kuhusu jambo hili kwani wanatambua siku chache zijazo Iniesta na Xavi wataishiwa viwango hivyo Thiago ndiye atakuwa mbadala sahihi kwa kwenye namba za wachezaji hawa ndiyo maana wanaendelea kung'ang'ania abaki lakini jitihada zao zinaweza kufikia ukingoni msimu huu kwani Thiago ameshaonesha nia ya kujiunga na Manchester United. Man utd inamtaka Thiago ili aweze kuimarisha safu ya kiungo baada ya Scholes kustaafu. Kamati ya usajili ya Manchester United imeshawasili nchini Hispania kuongea na wakala wa Thiago ikiwemo kupitia mkataba wake na Barcelona ili kupata njia ya kumsajili mchezaji huyo. Thiago Alcantara msimu huu amecheza mechi 25 za ligi na mechi mbili tu za Uefa Champions na asilimia kubwa ya mechi alizocheza amekuwa akitokea benchi akimpokea Xavi, Iniesta, Cesc au Pedro jambo hili ndilo linamuumiza kichwa kwani anaamini yeye ni mchezaji mwenye kiwango sawa na wenzake. 

No comments:

Post a Comment