Thursday, June 27, 2013

Klabu ya Yanga kuanza ziara kanda ya Ziwa

Timu ya Young Africans inatarajiwa kwenda kanda ya Ziwa mwishoni mwa wiki ijayo kwa ajili ya kucheza michezo ya kirafiki ya kujiandaa na maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu 2013/2014, ambapo itatumia fursa hiyo pia kuwaonyesha  kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom na kusherehekea pamoja na wapenzi, washabiki na wanachama wake. Akiongea na waandishi wa habari makao makuu ya klabu ya Yanga, mkurugenzi wa kampuni ya Nationwide ambao ndio waandaji wa ziara hiyo Frank Pangani amesema wao wanatumia fursa hiyo kwa wakazi wa kanda ya ziwa kupata fursa ya kuwaona wachezaji wa Yanga wakiwa na kombe lao la Ubingwa wa Vodacom pamoja na kushuhudia michezo ya kirafiki ya kimataifa. Naye Afisa Habari wa klabu ya Yanga Baraka Kizuguto amesema ziara hiyo wataitumia kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom, wanachama na wapenzi wa Yanga kuliona kombe la Ubingwa ikiwa ni pamoja na kucheza michezo ya kirafiki ambayo mwalimu ataitumia kwa ajili ya kukiandaa kikosi chake. Ziara ya Mabingwa au Champions Tour ni tukio la kila mwaka linalowahusisha mabingwa wa soka wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na mabingwa wa soka waalikwa wa kutoka nchi jirani za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na pia timu alikwa ya nyumbani. Mechi za Ziara ya Mabingwa mwaka huu wa 2013 zitachezhwa katika mikoa ya Mwanza (CCM Kirumba) Jumamosi 06/07/2013 Yanga vs KCC, Shinyanga (CCM Kambarage) Jumapili 07/07/2013 Yanga vs KCC marudiano, na Tabora (Ali Hassan Mwinyi) Alhamisi 11/07/2013 Yanga vs timu ya nyumbani itakayotangazwa siku mbili zijazo. Baada ya mechi hizo ziara hiyo inatarajiwa kuendelea katika mikoa itakayotanagazwa baadae.

No comments:

Post a Comment