Tuesday, April 23, 2013

Rais wa Bayern atuhumiwa kukwepa kodi

Kansela Angela Merkel amefadhaishwa na kashfa ya kukwepa kodi inayomkabili rais wa timu ya mpira wa miguu ya Bayern Munich, Uli Hoeness. Kwa mujibu wa msemaji wa kansela Seibert, Kansela Merkel amefadhaishwa sana na jambo hili kutokana na ukweli kwamba Hoeness amekuwa kielelezo chema kwa Ujerumani, kwani sio tu kwamba anaongoza klabu bora kabisa ya mpira, bali pia amekuwa akiunga mkono jithada kadhaa za maendeleo, ukiwemo mradi wa kuwajumuisha wageni kwenye jamii ya Ujerumani. Jambo hili ambalo limesharipotiwa kwenye vyombo vya dola kwa uchunguzi zaidi mwendesha mashitaka Mkuu wa Munich, Ken Heidenreich, amethibitisha kuendelea kwa uchunguzi dhidi ya Höness, ingawa hakutaja kiwango cha fedha kinachohusika wala muda ambao uchunguzi huo utachukua.Hata hivyo, Hoeness, mwenye umri wa miaka 61, amesema hana mpango wowote wa kujiuzulu kutokana na tuhuma hizo za kukwepa kodi.
Badala yake, rais huyo wa Bayern Munich, ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya timu hiyo, ameliambia gazeti la Sport Bild Plus, atahudhuria kweye mechi ya nusu fainali ya Champions League kati ya timu yake na Barcelona hapo kesho. Mwenyewe Hoeness, ambaye pia ni mmiliki mwenza wa kiwanda cha kusindikia nyama, amekataa kuingia undani wa suala hili, lakini ameahidi kutoa ushirikiano wowote unaohitajika kwa waendesha mashitaka.
Ripoti hizo za kukwepa kodi ndizo zilizohanikiza kwenye vyombo vya habari nchini Ujerumani na Hoeness amenukuliwa na gazeti la Münchener Merkur, kwamba atajitetea kisheria dhidi ya vyombo vya habari viinavyomtuhumu.
Höness, ambaye mwenyewe ni mchezaji wa zamani wa Ujerumani ya Magharibi, amekuwa msemaji mkubwa kwenye soka ya Ujerumani, Bundesliga. Alikuwa meneja wa kwanza kijana kabisa kwenye Bundesliga, baada ya kuchukua nafasi hiyo akiwa na miaka 27 tu, kufuatia jeraha lililohitimisha uchezaji wake uwanjani.
Baada ya zaidi ya miaka 30 akiwa kama meneja wa kibiashara wa Bayern Munich, mwaka 2009 alimrithi Franz Beckenbauer kama rais wa timu hiyo. Chini ya uongozi wake, klabu hiyo imekuwa na mafanikio zaidi kuliko klabu zote za mpira nchini Ujerumnai na moja ya klabu tajiri kabisa duniani. Habari hizi ni kwa mujibu wa DW

No comments:

Post a Comment