Thursday, May 30, 2013

Balozi wa Tz Ethiopia aongea na Taifa Stars

Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Joram Biswaro amewataka wachezaji wa Taifa Stars kuhakikisha wanaipeleka timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil. Ametoa changamoto hiyo wakati alipotembelea mazoezi ya timu hiyo jana (Mei 29 mwaka huu). Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imepiga kambi nchini Ethiopia na inafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Addis Ababa. “Watanzania tunafurahi kutokana na uwezo mnaouonyesha, hasa baada ya kuifunga Morocco mabao 3-1. Kama mliwafunga nyumbani hata kwao mnaweza kuwafunga. Tunataka kuwaona Maracana (Brazil) mwakani, mimi tayari ninayo tiketi mtanikuta kule,” amesema Balozi Biswaro ambaye enzi zake aliwahi kuichezea timu ya Yanga.
Taifa Stars ambayo iko Addis Ababa tangu Jumatatu (Mei 27 mwaka huu) imeweka kambi katika hoteli ya Hilton ambapo Jumapili (Juni 2 mwaka huu) itacheza mechi ya kirafiki na Sudan (Nile Crocodile) kwenye Uwanja wa Addis Ababa. Balozi Biswaro ameikaribisha Taifa Stars ubalozini Addis Ababa mara baada ya mechi dhidi ya Sudan ambapo itakutana na baadhi ya Watanzania wanaoishi Ethiopia kabla ya kuondoka alfajiri kwenda Marrakech, Morocco kwa kupitia Cairo, Misri.

No comments:

Post a Comment