Tetesi za usajili wa Thiago Alcantara, kiungo wa Barcelona, bado zinachanganya watu kutokana na taarifa tofauti zilizopo kwenye vyombo vya habari hadi sasa. Vyombo vingi vya habari vya kimataifa hususani vya nchini Uingereza na Hispania vinaripoti kuwa, usajili wa Thiago umefikia mwisho na mchezaji huyo anatarajiwa kutangazwa rasmi na Man utd wiki ijayo akiwa kama mchezaji wa kwanza kusajiliwa na David Moyes. Taarifa hizi zimetolewa na Geoff Sweet wa The Sun pamoja na Espana gazeti la Hispania, kwa pamoja magazeti haya yenye taarifa za kuaminika yamethibitisha kukamilika kwa usajili wa Thiago Alcantara kwenda Man utd. Lakini mkanganyiko wa usajili wa Thiago unakuja kwa taarifa za klabu ya Barcelona zilizosema Thiago hauzwi, na wakati huo huo Rafina Alcantara ndugu wa Thiago anayechezea Barcelona, naye alisema kuwa Thiago atabaki Barcelona, kabla ya Thiago mwenyewe kuandika kwenye akaunti yake ya Twitter wiki iliyopita akisema ‘naipenda Barcelona’. Hata hivyo, kitendo cha Thiago kusema anaipenda Barcelona, inaweza kuwa ni danganya toto ya mchezaji huyu ili asiweke mazingira mbaya ya kuondoka Barca au asionekane mbaya pindi akishindwa kuondoka. Vilevile, taarifa hizi za kusema anaipenda Barca, sio za kuaminika asilimia 100, kwani Thiago mwenyewe ndiye aliyeanza kuonesha hali ya kutoridhishwa na mazingira yaliyopo ndani ya klabu ya Barcelona. Thiago alipewa ahadi ya kupata namba ya uhakika msimu uliopita kwenye kikosi cha kwanza, lakini akajikuta akianza kwenye kikosi cha kwanza mara 20 tu kati ya mechi zaidi ya 50 ambazo Barca ilicheza msimu uliopita. Hali hii, ndiyo ilipelekea Thiago kwa kupitia wakala wake kutangaza nia ya kuhama Barca na kufanya klabu za Man utd, Arsenal na Tottenham kuonesha nia ya kumsajili, lakini hadi sasa, klabu ya Man utd pekee ndiyo ipo kwenye nafasi nzuri za kumsajili mchezaji huyu na kama taarifa za magazeti The Sun na Espana ni za kweli, basi Thiago atatangazwa rasmi kuhamia Man utd wiki ijao.
No comments:
Post a Comment