Saturday, March 15, 2014

Yanga yapata droo na Mtibwa Sugar mjini Moro


Yanga

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara timu ya Young Africans leo imetoka suluhu (0-0 ) dhidi ya timu ya Mtibwa Sugar ya Manugu katika mchezo uiofanyika jioni ya leo dimba la Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Young Africans ikicheza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu kwa takribani wiki mbili baada ya kutolewa katika mashindano ya kimataifa iliwakosa wachezaji wake wanne mlinda mlango Deo Munish "Dida" ambaye ni majeruhi, Mbuyu Twite (ruhusa), Haruna Niyonzima (malaria) na Mrisho Ngasa (majeruhi). 

Katika mechi ya leo mjini Morogoro, mchezo ulikosa radha kwa timu zote kutokana na mvua kubwa zilizoyesha mjini Morogoro na kusababisha wachezaji kushindwa kuonyesha ufundi wao na kujikuta mara nyingi wakiteleza na kukosa mipira au mipira kuwapita na kutoka nje. Washambuliaji wa Young Africans walifanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Mtibwa Sugar kupitia kwa washambuliaji wake Emmanuel Okwi, Didier Kavumbagu, Saimon Msuva na Hamis Kizza lakini walikuta mipira yao ikiokolewa na walinzi wa Mtibwa Sugar au kutoka sentimeta kadhaa pembani ya lango. Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza, zinamalizika, Mtibwa Sugar 0 - 0 Young Africans.


Mtibwa

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko Young Africans wakiwaingiza Hassan Dilunga, na Hussein Javu kuchukua nafasi za Nizar Khalfani na Hamis Kizza mabadiliko ambayo yaliongeza uwezo wa kumiliki mpira na kufanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Mtibwa Sugar. Dakika ya 82, 84, 87, 89 na 90 Young Africans ilikosa nafasi za wazi za kuweza kujipatia bao kupitia washambuliaji wake Okwi, Didier na Javu baada ya mipira waliyoipiga kuokolewa na golikipa Sharrif na mwingine kugonga mwamba na kutoka nje na kuwa kona ambazo hazikuzaa matunda.

Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Mtibwa Sugar 0 - 0 Young Africans. Mara baada ya kumalizika kwa mchezo, kocha wa Young Africans Hans Van der Pluijm amesema vijana wake wamecheza vizuri ila timu yake leo haikua na bahati wamekosa nafasi zaidi ya tatu za kufunga, pia uwanja uliikosesha timu yake ushindi kutokana na matope na utelezi uliokua umejaa na kutokana na kunyesha kwa mvua. "Leo tumamaliza kwa kutofungana na Mtibwa Sugar, nguvu zetu tunazielekezea kwenye mchezo dhidi ya Azam FC siku ya jumatano katika uwanja wa Taifa, tunaamini tutafanya vizuri na kupata ushindi katika mchezo ili kupunguza tofauti ya pointi iliyopo kwa sasa baina yetu na wao" alisema Hans

Young Africans: 1.Kaseja, 2. Juma Abdul, 3.Oscar, 4. Cannavaro, 5. Yondani, 6. Domayo, 7. Msuva, 8. Nizar/Dilunga, 9. Didier, 10. Okwi, 11. Kizza/Javu 


Matokeo mengine ya ligi kuu ni kama ifuatavyo; 

FT: Azam FC 4-0 Coastal Union
FT: Kagera Sugar 2 : 1 Prisons FC

No comments:

Post a Comment