Monday, April 22, 2013

Nusu Fainali UEFA Champions

Wiki hii wapenzi wa soka duniani watashudia vigogo wa soka Hispania na Ujerumani wanakutana katika nusu fainali ya klabu bingwa ulaya (UEFA champions). Katika droo iliyofanyika tarehe 12/4/13, mchezo wa kwanza utakuwa ni kati ya Bayern Munich vs Barcelona na mchezo wa pili utakuwa ni Borussian Dortmund vs Real Madrid. Mashabiki wengi wa soka duniani walipenda kuona timu za nchi moja hazikutani kwenye nusu fainali kitu ambacho kimekuwa kweli, ili kujua ni nchi gani kati Ujerumani na Hispania wenye timu bora kwa sasa.

Uchambuzi wa MichezoUpdates unaonesha mwaka 2010 nchini Afrika ya Kusini katika nusu fainali za kombe la dunia Ujerumani na Hispania zilikutana katika mchezo mkali wenye upinzani ulioipa Hispania ushindi mfinyu wa goli moja kwa bila, katika mechi hiyo asilimia 90 ya wachezaji waliocheza kwa timu zote mbili Ujerumani na Hispania ndiyo waliopo hadi sasa kwenye vilabu hivi vinne vinavyokutana katika michuano ya nusu fainali, hii inaonesha vita ya Ujerumani na Hispania bado inaendelea na safari hii Wajerumani watahitaji kuondoa uteja kwa Hispania. Matokeo ya FIFA yaliyotolewa mwezi huu yanaonesha Hispania na Ujerumani bado wanafukuzana katika nafasi mbili za juu, Hispania ikiwa ya kwanza na Ujerumani ya pili. Mambo haya mawili ni kielelezo cha kwanza kinachoonesha utamu wa mechi hizi za nusu fainali UEFA champions.Kielelezo cha pili kinaonesha Bayern Munich na Barcelona ndiyo timu zinazoongoza katika ligi za Ujerumani na Hispania zikiwa na tofauti kubwa dhidi ya wapinzani wao walipo nafasi ya pili ambao ni Bourussia Dortmund na Real Madrid. Hivyo kwa nusu fainali hii inawakutanisha washindi wa kwanza na wapili kwenye ligi za Hispania na Ujerumani. 

Wakati vuguvugu la nusu fainali likiwa limepamba moto kocha wa Bayern Munich Heynckes amesema hana mpango wa kuomba ushauri kwa kocha wa zamani wa Barcelona Pep Guardiola ambaye ameshasaini mkataba wa kuifundisha Munich msimu ujao. Heynckes aliyasema hayo alipokuwa anaongea na jarida la “Goal” baada ya kuulizwa kama atampigia simu Pep kumuomba ushauri, alisema “naomba mniheshimu mimi na kazi yangu, siwezi kufanya kitendo kama hicho”. Lakini ukweli halisi wa kauli hiyo hauwezi kujulikana kwasababu Pep anaijua Barcelona nje ndani, na ni kweli atakuwa msaada mkubwa kwa benchi la ufundi la Bayern kuweza kuwapa ushauri wa nini cha kufanya.

Mourinho kocha aliyeweza kushinda kombe la UEFA mara mbili akiwa akiwa na timu tofauti ya Porto na Inter Milan, ataweka rekodi katika michuano hii kama atafanikiwa kuiwezesha Real Madrid kuchukuwa ubignwa wa UEFA msimu huu, akiweza kufanikisha hilo Mourinho atakuwa ni kocha wa kwanza kushinda kombe hilo akiwa na timu tatu tofauti. Jose Mourinho ambaye anatarajiwa kurudi Chelsea msimu ujao atahitaji kuondoka Real akiwa na rekodi nzuri ikiwa ni pamoja na kushinda UEFA champions kombe ambalo Real wamelikosa kwa miaka kumi na moja sasa. Borussia Dortmund ikiwa ni timu ambayo haijafika kwenye nusu fainali kwa muda mrefu imefurahi kukutana tena na Real Madrid timu ambayo walikuwa wote kwenye hatua ya makundi ambapo Dortmund waliweza kushinda 2-1 wakiwa nyumbani na kutoka droo ya 2-2 Santiago matokeo ambayo yaliifanya Dortmund iongoze katika kundi hilo la kifo lililojumuisha mabingwa wa England (Man city), Spain (Real Madrid) na Holland (Ajax).

Barcelona timu ambayo inachukuliwa kuwa ndiyo timu bora duniani imekuwa na presha kubwa ya kurudisha hadhi yake toka mwaka 2011 iliposhinda kombe hili mara ya mwisho chini ya Pep Guardiola. Kumekuwa na fikra tofauti kuwa Barcelona imeishiwa baada ya Pep kuondoka na wengine wakisema muda wao wa kutamba umekwisha licha ya kuendelea kuwa tishio kwa timu pinzani lakini wao Barcelona wanaamini timu yao ni kama zingine hivyo inaweza kushinda au kufungwa licha ya kuwa mwaka huu wanauchukulia kama ni wao ikiwa ni kumbukumbu ya kurudi tena Wembley kwenye uwanja walioshinda kombe hili kwa mara ya mwisho 2011. Kocha wa Barcelona amekuwa nje ya uwanja kwa kipindi akitibiwa kansa kitu ambacho kiliwaathiri Barca kwa kiasi kikubwa na kupelekea kupata matokeo mabaya katika baada ya mechi, hali ya kuugua na kupata nafuu kwa kocha wao kumewafanya wachezaji wajiunge kwa pamoja na kuweka ahadi ya kujitahidi kufa na kupona ili wampatie zawadi ya kombe hilo Tito Vilanova kama ambavyo walivyofanya kwa Eric Abdial mwaka 2011.

Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Robert Lewandowski na Thomas Muller ni majina ambayo tunategemea kuyasikia zaidi katika nusu fainali wakiwa ndiyo wachezaji tegemezi kwa timu hizi nne. Wachezaji hawa pamoja na wengine muhimu wameonekana kupumzishwa kwenye michezo ya ligi kungojea siku ya tarehe 23 na 24 April ambapo nusu fainali ya kwanza itachezwa jijini Munich na Durtmund nchini Ujerumani.

Washibiki wengi duniani wamekuwa na fikra za kuona Clasico kwenye fainali yani Barcelona vs Real Madrid ikiwa ni timu zenye upinzani mkubwa na zinacheza mpira unaovutia, lakini kutimia hayo ni baada ya Real Madrid kumaliza shughuli pevu kuwatoa Dortmund timu ambayo ilishawapa kichapo cha goli 2-1, wakati Barcelona wao watatakiwa kuomba Messi, Xavi,Busquets na Iniesta wawe kwenye fomu ya uhakika ili waweze kuvunja ngome ya ‘The Bavarians’ ili kufika fainali. 

No comments:

Post a Comment