Friday, May 10, 2013

Manyara na Kiluvya nje kwenye michuano ya mikoa

Wakati Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) inaanza kutimua vumbi keshokutwa (Mei 12 mwaka huu), timu mbili zinakwenda moja kwa moja raundi inayofuata baada ya mabingwa wa Pwani, Kiluvya United kuondolewa na mkoa wa Manyara kutowasilisha bingwa wake. Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Mei 10 mwaka huu) imeiondoa Kiluvya United baada ya kubaini kuwa timu hiyo haikushiriki ligi ya mkoa wala wilaya msimu uliopita, hivyo kutokuwa na sifa ya kucheza ligi ya Mkoa msimu huu. Hivyo Friends Rangers ya Dar es Salaam iliyokuwa icheze na Kiluvya United na Mpwapwa Stars ya Dodoma iliyokuwa iwakabili mabingwa wa Manyara zinakwenda moja kwa moja raundi ya pili. Timu nyingine iliyokwenda moja kwa moja raundi ya pili itakayochezwa kati ya Mei 25 na 25 mwaka huu na mechi za marudiano ni kati ya Juni 1 na 2 mwaka huu ni mabingwa wa Shinyanga, Stand United FC. Kamati hiyo iliyokutana chini ya uenyekiti wa Blassy Kiondo pia imeagiza viongozi wa mikoa ya Manyara na Pwani waandikiwe barua za onyo kwa kushindwa kuwasilisha majina ya mabingwa wao. Vilevile imesisitiza viwanja vitakavyotumika kwa mechi za RCL ni vya makao makuu ya mikoa tu, isipokuwa kwa Uwanja wa CCM Mkamba ulioko Ifakara, Morogoro ambao ulishakaguliwa na TFF, hivyo kutumika kwa michuano ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu huu. Pia usajili unaotumika katika RCL ni ule ule wa ligi ya mkoa

No comments:

Post a Comment