Saturday, May 11, 2013

Yanga wapiga kambi Pemba kujiandaa na Simba

Kikosi cha mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2012/2013 timu ya Young Africans Sports Club leo asubuhi kimeanza mazoezi katika uwanja wa Gombani mjini Pemba kujiandaa na mchezo wake wa mwisho dhidi ya timu ya Simba SC, mchezo utakaofayika mei 18 katika dimba la uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam. Yanga ambayo tayari ilishatwaa Ubingwa wa VPL kabla hata ya Ligi kumalizika imewasili salama kisiwani Pemba ambapo leo asubuhi kocha mkuu Ernie Brandts ameongoza mazoezi ya kikosi hicho kinachojiwinda kupata pointi 3 dhidi ya Simba Sc. Ikiwa imebakia takribani wiki moja kabla ya mchezo wenyewe kufanyika, uongozi wa klabu ya Yanga kwa kushirikiana na benchi la ufundi uliamua kubadilisha mazingira ya kambi kutoka makao makuu ya klabu mpaka kisiwani Pemba kuhakikisha wachezaji wanapata mafunzo katika hali iliyo tulivu zaidi. 
Akiongea mara baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, kocha Brandts amesema amefurahishwa kwa mapokezi ya wakazi wa kisiwa cha Pemba, kwani licha ya kuja kuweka kambi ya kujianda na pia wamepata fursa ya kubadilisha mazingira na kujifua vizuri katika hali iliyo tulivu. Kuhusiana na hali ya kikosi Brandts alisema kikosi chake kipo fit kiakili, kifikra na morali ya hali ya juu kuelekea kwenye mchezo hali inayoendelea kumpa uhakika zaidi wa kuondoka na pointi 3 katika mchezo huo wa mei 18.Aidha Brandts akliongeza kuwa wachezaji wake wote wapo salama, hakuna mgonjwa wala mchezaji majeruhi hivyo kuja kuweka kambi kisiwani Pemba kumeniongezea fursa ya kukaa na wachezaji wangu wote kwa pamoja, kuwapa mbinu mbalimbali kwa pamoja na kupanga jinsi ya kuibuka na ushindi dhidi ya Simba SC. Uogozi wa klabu ya Yanga unawaomba wapenzi, wanachama na washabiki wake wote kwa pamoja kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa mei 18 dhidi ya Simba Sc kwani licha ya kucheza na watani wa jadi pia itakua ni siku ambayo Yanga itakabidhiwa rasmi kombe la Ubingwa wa VPL 2012/2013.

No comments:

Post a Comment