Thursday, January 23, 2014

Yanga kuondoka Uturiki leo mchana

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara timu ya Young Africans imeendelea na mazoezi ya asubuhi katika viwanja vya hoteli ya Sueno  katika kuendelea kujiweka sawa kabla ya kuanza safari kesho mchana ya kurejea nchini Tanzania tayari kwa mikikimikiki ya mzunguko wa pili wa VPL 2013/2014.

Kocha mkuu Hans Van Der Plyum ameendelea kuwaandaa wachezaji wake na kuyafanyia marekebisho kadhaa yaliyojitokeza katika mchezo uliopita dhidi ya Simurq PIK kabla ya kesho kuanza safai ya kurejea nyumbani tayari kwa kufungua dimba siku ya jumamosi dhidi ya Ashanti United.

Katika mazoezi ya leo asubuhi kocha Hans amesema kikosi chake kinaendelea vizuri mpaka sasa, hakuna majeruhi na wachezaji wanajituma na kuwajibika kwa kujua wajibu wao ni nini hivyo inakua rahisi pia kushika maelekezo yake.

Mara baada ya mazoezi ya asubuhi kocha Hans amesema timu itaendelea tena na mazoezi ya jioni kuanzia majira ya 9:30 kwa saa za huku sawa na 10:30 kwa saa za Afrika Mashariki ambapo hayo ndo yatakua mazoezi ya mwisho kabla ya kesho kuanza kwa safari ya kurejea Tanzania.

"Nina uzoefu na soka la Afrika takribani kwa miaka 15, wachezaji niliowakuta hapa Young Africans wana uwezo mzuri wote, wanajituma, wana nidhamu na upendo wa hali ya juu kitu ambacho kwa mwalimu yoyote lazima atafurahia mazingira hayo kwani hata ufanyaji wake kazi unakua mzuri "alisema Hans." 

Aidha Hans ameongeza kwa siku tisa alizokaa na wachezaji wake Sueno Hotel Beach Side Antalya katika mazoezi na mafunzo aliyokuwa anawapatia anaamini sasa timu yake ipo tayari kutetea Ubingwa wa Ligi pamoja na kufanya vizuri kwenye na mashindano ya kimataifa .

Kambi ya siku 14 katika hoteli ya Sueno Beach Side  Manavgat jijini Antalya imekua nzuri sana kwani wachezaji na benchi la ufundi kwa ujumla wameweza kutimiza wajibu wao ambapo dhumuni kubwa ilikua ni kufanya mazoezi, kupata michezo ya kirafiki kwa ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili VPL na mashindano ya Klabu Bingwa barani Afrika. 

Young Africans ambayo imeweka kambi nchini Uturuki kwa takribani siku 14 mpaka sasa, iliweza kucheza michezo minne ya kirafiki dhidi ya timu za Ankara Sekerspor na Altay SK za Ligi Daraja la pili nchini Uturuki kabla ya kuivaa timu ya KS Flumartari ya Albania kisha kumaliza na timu ya Simurq PIK ya Azerbajain.

Matokeo ya mechi hizo ni:

11.01.2014

Young Africans 3 - 0 Ankara Sekerspor

(Didier 10, Okwi 46,  Kiiza 61)

15.01.2014

Young Africans 2- 0 Altay SK

(Didier 46, Okwi 57)

18.01.2014

Young Africans 0 - 0 KS Flumartari

20.01.2014

Young Africans 2 - 2 Simurq PIK

(Didier 13, Ngasa 30)  -  (Anderson 45, Sattarli 56)

No comments:

Post a Comment