Friday, July 12, 2013

Poulsen na Micho waahidi kupambana mechi ya leo

Makocha Kim Poulsen wa Taifa Stars na Sredojvic Micho wa The Cranes wamesema mechi ya leo baina ya timu hizi (kwenye michuano ya CHAN) itakuwa ngumu kwa vile kila mmoja amejiandaa kuhakikisha anafanya vizuri. Wakizungumza na Waandishi wa Habari jana, makocha wote walielezea ubora wa wapinzani wao, lakini wakasisitiza kuwa wanaingia uwanjani kuhakikisha wanashinda ili kujiweka katika mazingira mazuri kwa ajili ya mechi ya marudiano itakayochezwa Kampala wiki mbili zijazo. Kim alisema Uganda ndiyo inayoongoza kwa ubora wa viwango vya FIFA katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo ni changamoto kwao ingawa wachezaji wake tayari wamejipanga vizuri kwa ajili ya mechi hiyo. Naye Micho aliyefuatana na nahodha wake Hassan Wasswa alisema Taifa Stars imekuwa ikifanya vizuri tangu iwe chini ya Kim, na itakuwa na wachezaji tisa wa kikosi cha kwanza kinachocheza mechi za mchujo za Kombe la Dunia wakati kwa upande wake atakuwa na wachezaji wawili tu, hivyo anawachukulia Stars kama ni timu itakayowapa upinzani mkubwa licha ya kuwa baadhi ya wadau wametafsiri kauli hiyo kama danyanya toto. Mechi kati ya timu hizi itachezwa leo jioni kuanzia saa tisa katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam. 

No comments:

Post a Comment